Breaking

Monday, April 6, 2020

Spika Ndugai Kuanika Hadharani Madeni ya Wabunge, Amemtaka Lissu Kulipa Deni Lake la Sh Milioni 70


Spika wa Bunge Job Ndugai ameahidi kuweka wazi madeni na madai ya wabunge wote ifikapo Juni 30 mwaka huu na kudai kuws waliowengi kiinua mgongo chao kitakuwa kidogo.

Kadhalika, amemtaka aliyekuwa Mbunge wa Singida Mashariki Tundu Lissu kulipa madeni anayodaiwa ya Sh.Milioni 70 aliyokopa maeneo mbalimbali kupitia Bunge.

Akizungumza mara baada ya kupitishwa bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka 2020/21, Spika Ndugai amesema hadi kufikia Juni 30, mwaka huu kila kitu kitawekwa hadharani vizuri kimahesabu huku akisema waliowengi kiinua mgongo chao kitakuwa ni kidogo.

“Madeni ni mengi sana, kila mmoja apige hesabu madai aliyonayo na madeni, kuwa na madeni makubwa ni kukosa sifa ya uongozi, msiangalie bajeti ya Waziri Mpango na kuikosoa wakati ukiangalia mtu ameshindwa bajeti yake tena kwa mbali,”alisema.

Kuhusu Lissu, alisema amelipwa mishahara yake yote ikiwemo wa Juni 2019 ambayo anadai hajalipwa.

“Mishahara yote zaidi ya Sh. Milioni 200 amelipwa anadai wapi, wakati mwingine mtu awe na shukrani, posho mbalimbali zaidi ya Sh.Milioni 360 badala ya kunituhumu tuhumu, kwa ujumla amelipwa zaidi ya Sh.Milioni 500 kwa kipindi alichokuwepo,”alisema

Amesema Lissu ana mikopo ambayo amechukua maeneo mbalimbali na kumtaka arejeshe fedha hizo huku akisema si vyema kuwekwa mambo ya mtu hadharani lakini inalazimika kutokana na yeye kujitokeza kwenye mitandao.

Hata hivyo, amesema kama ataendelea wataenda mbali na kuhoji jinsi alivyotumia fedha za wananchi, mishahara ya dereva wake na mafuta ya kumpeleka jimboni huku akijua kuwa anaitumia isivyo halali kwa sababu yupo nje ya nchi jambo ambalo litamletea shida kwa kutakiwa kuzirudisha.

“Mishahara ya dereva, mafuta ya kumpeleka jimboni na posho alipokea akiwa ubelgiji,”amesema.

 HIZI HABARI ZA HIVI ZINAPATIKANA GODSTAR ONLINE >>BONYEZA HAPA KUDOWNLOAD APP YA GODSTAR ONLINE

No comments:

Post a Comment