Breaking

Friday, April 3, 2020

Ushauri Mzito Watolewa Kifo Cha Corona Bongo


KUFUATIA kifo cha kwanza nchini kilichosababishwa na virusi vya Corona, Daktari wa Hospitali ya Temeke jijini Dar, Dk Godfrey Chale ametoa ushauri kwa watu waliokuwa karibu na marehemu ili kuhakikisha ugonjwa huo hauzidi kusambaa.

 

Akizungumza na Risasi Mchanganyiko jana mara baada ya kuripotiwa kwa kifo hicho cha kwanza nchini, Dk Chale alisema watu wote waliokuwa karibu na marehemu kwa siku kadhaa kabla ya kifo, wanapaswa kujitokeza na kuwekwa chini ya uangalizi kama anavyohimiza waziri wa Afya, Ummy Mwalimu.

 

“Wanatakiwa wao wenyewe kujitokeza, kukaa chini ya uangalizi lakini wakati huohuo watachukuliwa vipimo vya kubaini kama wana maambukizi ya Corona au la. Hili ni suala ambalo linahitajika kufanyika haraka na kwa umakini mkubwa maana hatujui marehemu amekutana na nani kabla hajagundulika kupata virusi vya Corona,” alisema daktari huyo.

 

Dk Chale pia amezidi kuwataka Watanzania kuchukua tahadhari ambazo zimeshatolewa na Serikali ikiwemo kuepuka mikusanyiko isiyokuwa ya lazima, kunawa kwa maji safi yanayotiririka na sabuni au vitakasa mikono lakini pia kutosafiri safari ambazo hazina ulazima.

 

“Na unapojisikia dalili zozote za kuumwa homa kali na mafua au kukohoa ni vyema sana kutoa taarifa hospitali ili kuweza kupata msaada,” alisema.

 

Taarifa iliyotolewa jana na Waziri wa Afya wa Tanzania, Ummy Mwalimu imethibitisha kifo hicho na kubainisha kuwa alikuwa akipatiwa matibabu katika kituo cha matibabu ya wagonjwa wa Covid-19 kilichopo Mloganzila.

 

“Marehemu ni Mtanzania mwanaume mwenye umri wa miaka 49 ambaye pia alikuwa akisumbuliwa na maradhi mengine. “Tunamuomba Mungu ailaze roho yake mahala pema peponi, na tunatoa pole kwa familia, ndugu jamaa wa marehemu,” alisema Ummy. Alisema hadi jana asubuhi, watu 20 wameambukizwa Corona, aliyepona ni mmoja na kifo ni kimoja.


HIZI HABARI ZA HIVI ZINAPATIKANA GODSTAR ONLINE >>BONYEZA HAPA KUDOWNLOAD APP YA GODSTAR ONLINE 

No comments:

Post a Comment