Breaking

Tuesday, January 28, 2020

HADITHI: NIMEKOSA NINI? sehemu ya 2

Image result for NIMEKOSA NINI

Na. Godfrey Godstar.
ILIPOISHIA....
“Halafu linaonekana ni tukio kubwa sana, yaani mpaka polisi wamekuja!” Nilijiwazia huku nikitembea kwa tahadhari kuelekea ofisini.
SASA ENDELEA...
Kabla sijajichanganya kwenye umati wa watu niliamua kumuuliza jamaa mmoja ambaye alikuwa pembeni akivuta sigara yake, naona aliamua kujitenga pembeni kidogo ili aendelee kuunguza mapafu yake peke yake bila kumbughudhi wala kumkera binadamu mwingine kwenye huo mkusanyiko.
“Habari za asubuhi kaka!” Nilimpa hai kama ilivyo kwa mtu muungwana kama mimi.
“Safi tu ndugu yangu!” Alijibu jamaa huyo kisha akaitikisa sigara yake, kitendo ambacho kilisababisha idondoshe majivu ilipokuwa imechomeka. Wakati naendelea kumuongelesha aliipeleka tena mdomoni na kupiga pafu moja huku akinisikiliza kwa makini.
“Hivi kuna nini hapo, maana watu wamejazana na si kawaida yake?” Nilimswalika tena bwana masigara.
Kabla hajanijibu alipuliza moshi wa sigara kwanza ndipo akatoa jibu la swali nililokuwa nimemuuliza.
“Pamevamiwa usiku wa kuamkia leo!” Aliongea kisha akapiga pafu kadhaa mfululizo kisha akatupa filta ya sigara aliyokuwa akivuta maana ilikuwa imeshaisha.
Nilipofika kwenye umati ule nikaanza kuangaza angaza ili nimuone bosi wetu ama mfanyakazi mwenzangu yeyote ili nipate kumuulizia kwa kinaga ubaga juu ya tukio lililokuwa limetokea kwenye ofisi yetu hiyo.
Hata hivyo sikuweza kumuona mtu yeyote niliyekuwa namfahamu. Nikapenyapenya mpaka nikafanikiwa kufika wenye mlango wa kuingilia. Nikiwa hapo mlangoni niliweza kuisikia sauti ya bosi wetu ikilalamika mle ndani,
“Sikutegemea kabisa kama huyu kijana atatugeuka kiasi hiki, ukiangalia tabia yake na utendaji wake wa kazi haviendani kabisa na tukio hili alilolifanya, kumbe umdhaniae siye huwa ndiye.”
Kauli ile ilinifanya nianze kujiuliza,
“Inamaana tayari mwizi kashapatikana na tunafanya naye kazi kwenye hii hii kampuni, watu wengine sijui wakoje, yaani pa kulia yeye anapafanya msalani.” Nilijikuta nikikilaani sana kitendo kile huku sijui ni nani aliyekuwa amekifanya.
Kwa haraka haraka nikaanza kuwapima wafanyakazi wenzangu mmoja baada ya mwingine katika akili zangu kama kuna anayeweza kufanya upuuzi kama huo. Hata hivyo wote niliwaona ni waadilifu na wenye tabia njema.
“Labda mmoja kati yao shetani kamwingia na kujikuta anafanya utumbo kama ule!” Nilijiwazia mwenyewe. Wakati huo sasa akili yangu ilinituma niende huko ndani alikokuwepo bosi wetu ili nikazisikie habari zote kwa kina.
Niliingia nikamkuta bosi wetu akiwa na makachero kadhaa wakipekuapekua chumbani mle ambamo ndiyo ilikuwa ofisi ya bosi kubwa. Pale mezani kompyuta ya ‘marking tosh’ niliyozoea kuiona kila ninapoingia ofisini humo sikuiona siku hiyo. Akili yangu ikanituma kuwa huenda hata hiyo imebebwa na watu waliokuwa wanasemekana kuvamia.
“Habari za asubuhi bosi!” Nilitoa salamu kwa bosi wangu. Hata hivyo hakuongea chochote, kwa lugha nyepesi alinichunia. Nikaanza kujiuliza kwa nini sasa ananichunia? Au ndiyo kusema kachanganyikiwa na tukio la kuvamiwa au hajanisikia tu? Sikupata jibu.
Niliamua kurudia tena huku nikiongeza sauti ili kama hakusikia ile mara ya kwanza basi mara hii anisikie, kama ni kauzibe basi napo ningeweza kung’amua.
“Bosi nakusalimia!” Nilipayuka kwa sauti ya juu kiasi lakini bado mambo yalikuwa vilevile, tena safari hii aliniangalia na kunikazia macho kisha akaangalia pembeni, nadhani alitaka kunidhihirishia kabisa kwamba hata ile mara ya kwanza alikuwa kanisikia ila ila ‘alinikaushia’ tu.
Baada ya kuona hali hiyo niliamua kuwasalimia makachero waliokuwemo chumbani humo. Wao waliitikia wala hawakuninyamazia.
Mara nilimsikia bosi wangu akimwambia kachero mmoja aliyekuwa karibu naye,
“mtu mwenyewe ndiyo huyu!”
Niliposikia hivyo moyo wangu ulilipuka pu! Nilianza kujiuliza ni kitu gani mimi nimefanya.
“Kumbe ndiyo huyu!” aliongea afande huyo huku akinigeukia na kuniambia,
“bwana Jerry, kuanzia sasa upo chini ya ulinzi!” Aliniambia kachero huyo ambaye uso wake ulionekana kubadilika kwa wakati huo.
KWA NINI JERRY KAWEKWA CHINI YA ULINZI? USIKOSE SEHEMU INAYOFUATA!

No comments:

Post a Comment