Breaking

Monday, January 27, 2020

Historia ya mgunduzi wa Bunduki aina ya AK 47

Mbunifu wa bunduki aina ya AK 47, iliyomuua Rais Abeid Amani Karume
APRILI mwaka 1972, Rais Abeid Amani Karume wa Zanzibar, aliuawa akiwa anacheza bao na wanachama wa chama chake cha Afro Shiraz (ASP), katika Ofisi za Makao Makuu ya chama hicho eneo la Kisiwandui, Unguja.

Ni wachache wanaofahamu kwamba bunduki iliyotumika kumuua ilitengezwa nchini Urusi wakati huo na mtu aliyebuni silaha hiyo ambaye amefariki 2013 akiwa kijijini kwake huko Russia.

Ilikuwaje silaha iliyotengenezwa katika mojawapo ya vijiji vya Urusi ikafika Tanganyika na hatimaye kuvuka Bahari ya Hindi kwenda Zanzibar kutumia kumuua kiongozi huyo wa watu?
Je, mgunduzi wa silaha ambayo imesababisha mauaji ya mamilioni ya watu wasio na hatia duniani ni shujaa ama mhalifu?

Silaha iliyotumika kumuua Karume na mamilioni mengine ya watu inafahamika kwa jina la AK 47 Kalashnikov na dunia juzi imeomboleza kifo cha mtu aliyeigundua.
Mikhail Timofeyevich Kalashnikov (94) ameaga dunia juzi lakini ameiachia dunia urithi wa silaha ya bunduki aina ya AK 47 Kalashnikov; silaha inayoelezwa kuua watu wengi duniani kuliko nyingine yoyote.

Kalashnikov, aliyegundua silaha hiyo wakati wa Vita ya Pili ya Dunia, alifariki dunia kijijini kwake Izhevsk, baada ya kuugua kwa takribani mwezi mmoja kutokana na magonjwa mbalimbali yaliyosababishwa hasa na umri wake mkubwa.

Askari huyu wa aina yake katika karne iliyopita, aligundua silaha hii wakati alipokuwa akifanya kazi katika Jeshi la Urusi wakati huo na akiwa na umri wa miaka 22 tu.
Watu wengi wanadhani AK 47 iligunduliwa kwa kazi ya siku moja, lakini ukweli ni kwamba kazi ya kutengeneza na hatimaye kuimaliza silaha hii ilichukua muda wa takribani miaka sita ya majaribio.
Katika mahojiano aliyofanyiwa miaka minne iliyopita wakati alipokuwa akifanyiwa sherehe rasmi ya kutimiza miaka 90, Kalashnikov alisema hajutii kwamba silaha aliyobuni imeua watu wengi namna hiyo.
“Wakati nikitengeneza silaha hiyo, lengo langu halikuwa kuua mtu bali kulinda taifa langu. Kama baadaye imeanza kutumiwa na magaidi kuua watu, hilo halikuwa lengo langu.
“Hata hivyo, kusema ukweli ningefurahi zaidi kama ningeweza kubuni kifaa ambacho kingetumiwa na wakulima kwa namna ile ile ambayo AK 47 imetumika duniani kote. Pengine kwa namna hiyo ningeisaidia zaidi dunia,” alisema.

Hii ni silaha ambayo inapatikana karibu kote duniani. Kuna maeneo barani Afrika ambako watoto wa kiume wanaozaliwa huitwa Kalash kwa heshima ya silaha hiyo.
Katika baadhi ya bendera za taifa, silaha hii inaonekana. Nchi kama Zimbabwe na Burkina Fasso ni mfano wa nchi zilizoamua kabisa kuweka silaha hii kama mojawapo ya alama za taifa.
Katika soko la silaha leo, Kalashnikov (AK47) inaweza kupatikana nchini Afghanistan kwa thamani ya pauni tatu za Uingereza (shilingi elfu sita za Tanzania) na nchini India, silaha hiyo hiyo inaweza kupatikana kwa bei ya pauni 3,000 (shilingi milioni sita).

Kwa ujumla, rekodi zilizopo zinaonyesha kwamba kuna bunduki zaidi ya milioni 100 za aina ya AK 47 duniani kote. Kwa nini 47 zimekuwa maarufu sana?
Bunduki hizi ni mongoni mwa bunduki chache zilizopo duniani ambapo unaweza ukazizamisha kwenye maji na bado ikafyatua risasi kama kawaida.

Kalashnikov inaweza pia kufanya kazi katika mazingira yoyote. Iwe kwenye baridi kali kama ya Russia au joto kali kama la nchi zilizo jirani na ukanda wa Ikweta, AK 47 inafanya kazi zake bila ya matatizo.

Pia, silaha hii imejijengea sifa ya kuwa rahisi kujifunza kwani watu wanaoifahamu vizuri silaha hii wanasema mtu anaweza kufundishwa kuitumia katika muda wa saa nzima na akawa anaweza kuitumia.
Sifa nyingine iliyoipa umaarufu mkubwa silaha hii ni ile ya kuweza kusafishika kwa muda mfupi kuliko silaha nyingi zilizopo sasa na hii maana ya hii ni kwamba, haihitaji gharama kubwa kuifanyia matengenezo.

Umaarufu wa mgunduzi
Katika mahojiano aliyowahi kufanyiwa na jarida la Telegraph la Uingereza miaka kumi iliyopita, Kalashnikov alitoboa siri ya kwa nini ilimchukua muda mrefu kufahamika nje ya taifa lake ingawa silaha aliyoibuni ilikuwa maarufu nje ya Urusi.

“Kabla ya mwaka 1990, mimi nilifanywa siri na taifa langu. Sikuruhusiwa kusafiri nje ya Urusi kwa sababu yoyote ile bila ya serikali kufahamu. Inaonekana serikali ilihofu kwamba naweza kuibwa na uwezo wangu kutumikia mataifa mengine.

“Ni mpaka baada ya mwaka 1990 ndipo hasa nilipoanza kutoka nje ya Russia kwa kutumia jina langu halisi. Kabla ya hapo, hata niliposafiri nje ya nchi, nilikuwa nikitumia jina la bandia,” alisema.
Ni katika mahojiano hayo ndipo mgunduzi huyu alipowashangaza Waingereza kwa kuwaambia kwamba kwa maoni yake AK 47 si silaha bora kuliko zote zilizowahi kutengenezwa na kuwa ana imani ya kuwa ipo siku, itakuja silaha nyingine kubwa kuliko hiyo.

Kuna habari moja ya mzaha kati ya Kalashnikov na mgunduzi mwingine maarufu wa silaha katika Jeshi la Marekani, Eugene Stoner, aliyetengeneza bunduki aina ya M16. Kuna wakati walikutana nchini Marekani na kila mmoja akaanza kusifia ubora wa silaha yake.

Stoner alisema uzuri wa AK 47 unatokana na ukweli kwamba unabeba risasi nzito zaidi na hivyo uwezekano wa kuwa na shabaha ni mzuri kuliko Kalashnikov, lakini Mrusi huyo akajibu kwamba silaha nyepesi ni nzuri kwa sababu ni rahisi kubebwa.

Ubishi huo ulimalizwa katikati na mmoja wa makamanda wa majeshi ya Marekani ambaye alipomwona Kalashnikov, alimwambia; “Niliikumbuka sana bunduki yako wakati wa Vita ya Vietnam. Kama tungekuwa na AK 47 za kutosha, huenda vita ile ingekuwa na matokeo tofauti.”  Maneno hayo murua ya Jenerali huyo wa Marekani yalimaliza ubishi huo wa Stoner na Mikhail.
“Kusema kweli, sisi wagunduzi wa bunduki hatukuwa na nia mbaya hata kidogo. Ukiangalia kwa undani utaona kwamba lengo letu la kwanza lilikuwa ni kupambana na ufashisti.

“Lakini yaliyokuja baadaye ni maafa. Bunduki aliyoitengeneza Stoner ilitumika kuua raia wa Vietnam waliokuwa wakitetea uhuru wa taifa lao. Maafa makubwa. Bunduki iliyobuniwa na Uziel Gal (Uzi) imetumiwa sana kuua Wapalestina na jirani zao.

“Mimi nashukuru kwamba bunduki yangu niliyoibuni kuna watu wameifurahia. Sitasahau tukio moja lilitokea nchini Msumbiji ambapo viongozi wa serikali hiyo walinipa mwaliko kwa kusema; Kalashnikov, karibu nchini kwetu kwani bunduki yako ndiyo imetupa uhuru. Wapo askari ambao wamewapa jina la Kalash watoto wao wa kwanza wa kiume waliozaliwa baada ya ukombozi kwa sababu ya silaha hiyo,” alisema.

Kalashnikov na kubadili dini
Wakati mmoja, Kalashnikov alikuwa ametembelea nchini Saudi Arabia na alikuwa katika Uwanja wa Ndege wa Riyadh wakati mmoja na wenyeji wake alipozungumza neno ambalo limekuwa likirudiwa mara kwa mara.

“Mikhail, kwa nini usiamue tu kubadili dini kutoka Ukristo na kuwa Muislamu? Kwenye dini ya Kikristo, wewe unachukuliwa kama mtu uliyeua watu wengi na mdhambi.
“Lakini sisi katika dunia ya Uislamu, huku Mashariki ya Kati, jina lako linavuma. Hata bendera ya kundi linalochukuliwa kuwa la kigaidi la Hezbollah limeweka AK 47 kwenye bendera yake,” aliambiwa na mwenyeji wake huyo.

Kalashnikov alikataa ofa hiyo ya aina yake kwa upole. Kuna msemo katika ngano za kale za Urusi kwamba kubadili imani ya mtu ni kitu kigumu kwani imani si shati la kuvaa ambalo mtu anaweza kulibadili wakati wowote.

Amefaidika vipi na ubunifu wake?
Kutokana na majaribio aliyokuwa akifanya mara kwa mara ya bunduki zake, Kalashnikov alimalizia maisha yake ya uzeeni akiwa na nusu kiziwi. Ili kuzungumza na mgunduzi huyu, ilimpasa mtu kuzungumza naye akiwa jirani na sikio lake.

Na madhara haya hayakuwa kwake pekee. Wapo watu wengine ambao walikuwa wakiishi jirani naye kule kijijini kwake Izhev walioathirika na majaribio yake ya silaha ya mara kwa mara.
Kama mbunifu huyu angekuwa amezaliwa Marekani, leo angekuwa mmoja wa matajiri wakubwa lakini kwa sababu hakuweza kuiwekea silaha yake hiyo hatimiliki kwa sababu ya nchi yake kufuata sera za ukomunisti, amekufa akiwa mstaafu wa kawaida wa jeshi.

Mikhail alijiunga na Jeshi la Urusi miezi akiwa na umri wa miaka 19 tu. Yeye alikuwa mtoto wa mkulima tajiri ambaye hakupendwa na sera za ukomunisti na hatimaye yeye na familia yake wakafukuzwa kwao na kwenda kuishi Siberia.

Enzi ya utawala wa Kikomunisti wa Vladmir Lenin, familia yoyote iliyohamishiwa Siberia ilikuwa ni sehemu ya adhabu.

Walipokuwa Siberia ndipo kipaji cha ugunduzi cha Kalash kilipoanza kujulikana. Kwa sababu hakukuwa na mashine ya kusaga, kijana huyu mdogo alibuni mashine maalumu ya kusaga ambayo baadaye ilikuja kutumika kusagia mtama na ngano iliyokuwa ikitumiwa na wananchi wenzake.
“Shida na mateso ambayo familia yangu ilikuwa ikiyapata ndiyo yaliyonifanya nikawa mpambanaji wa kiwango cha juu. Nikajua, kama nisipokuwa mbunifu, kuna hatari ya familia yangu na mimi binafsi kuteketea,”alisema.

Hata hivyo, Kalashnikov anaamini kwamba alizaliwa na kipaji cha ugunduzi kwani tangu angali mdogo, siku zote alikuwa akibuni vitu adimu.

“Unajua ugunduzi ni sawa na kuwa mama mwenye mtoto tumboni. Ni lazima umchunge mwanao na uhakikishe anazaliwa akiwa salama. Unajua kosa lako moja tu linaweza kusababisha madhara kwa mtoto.

“Kama ugunduzi wako utauchukulia kwa umakini ule ule ambao mama mjamzito na anayelea mtoto mdogo anakuwa nao, uwezekano wa kuwa mgunduzi mzuri nao unaongezeka,” alipata kusema Kalashnikov.

Kuna wanaosema kwamba endapo Kalashnikov angezaliwa Marekani, huenda angevumbua silaha nyingi zaidi kutokana na namna teknolojia ilivyokua sana na uhuru uliopo pamoja na uwezeshaji ambao wagunduzi wanapewa wakiwa nchini humo.

Baadaye Mikhail aliamua kujiunga na Jeshi la Urusi ambako alijiunga katika kikosi cha Mizinga lakini wakati tayari akiwa ameanza kuonyesha uwezo wake kwenye eneo hilo, alipata shambulio lililoathiri bega lake na hivyo kutofaa tena.

Ni katika kipindi alipokuwa hospitali akiuguza jeraha lake hilo, ndipo Kalashnikov alipoanza kupata picha ya aina ya silaha anayotaka kuitengeneza. Silaha nyepesi kuibeba, inayoweza kumudu mazingira magumu, rahisi kutumia na yenye shabaha nzuri.

Ndipo hapo ilipozaliwa AK 47.
Kabla hajaibuni AK 47, zilipita aina nyingine tofauti za bunduki kama vile STi 444 ambayo ilitumika kidogo lakini haikuwa na umahiri wa kutosha lakini yenyewe ndiyo iliyofungua njia kwa Kalashnikov.
Bunduki iliyoua marais

Zaidi ya Karume, bunduki hii ya AK 47 pengine ndiyo yenye rekodi ya kuua marais wengi duniani kuliko nyingine yeyote.

Ni bunduki hii ambayo ilitumika kuondoa maisha ya aliyekuwa Rais wa Misri, Anwar Sadat mwaka 1981 katika tukio lilishuhudiwa na watu wengi.

Ni AK 47 Kalashnikov ndiyo iliyotumika kumuua aliyekuwa kiongozi wa Cape Verde, Amilcar Cabral, mwaka 1973 na kukatisha maisha ya mwanasiasa huyu anayechukuliwa mmoja wa viongozi bora kabisa kuwahi kutokea barani Afrika.

Ni bunduki hii hii iliyobuniwa na raia huyu wa Russia ambayo ilitumika kuondoa maisha ya Salvador Allende, aliyekuwa Rais wa Chile mwaka 1973 katika tukio ambalo bado linazungumzwa barani Amerika Kusini.

Ingawa hadi leo kuna utata kama Allende alijiua mwenyewe kwa kujipiga risasi au aliuawa na askari vibaraka wa Marekani waliokuwa wametumwa na Jenerali Augusto Pinochet (Mkuu wa Majeshi ya Chile wakati huo), lakini ushahidi wa kuaminika unaeleza ni AK 47 ndiyo iliyomuua.
Mwenyewe Allende alikuwa anamiliki bunduki ya aina ya AK 47 ambayo alikuwa amepewa kama zawadi na rafiki yake kipenzi, Fidel Castro, Rais wa Cuba wakati huo.

Majigambo ya AK 47
Baadhi ya viongozi wamekuwa wakiitumia silaha hii kuonyesha majigambo yao. Katika enzi alizokuwa Rais mwenye nguvu wa Irak, Saddam Hussein al Tikrit, alikuwa akipenda kufyatua bunduki yake aina ya AK 47 hadharani kwenye mikutano ya hadhara.

Mwenyewe alikuwa akipenda kufyatua risasi hewani huku akiwa ameishikilia bunduki yake kwa mkono mmoja.

Katika picha mbalimbali za televishenia alizokuwa akipiga na kutoa matamshi yake mbalimbali dhidi ya Marekani na vibaraka wake, Osama bin Laden , mara zote alikuwa akionekana huku akiwa na AK 47 yake pembeni.

Na hili sasa limeigwa pia na aliyekuwa namba mbili wake, Ayman al Zawahri.
Shujaa au Gaidi?

Wakati safari ya Mikhail Kalashnikov kwenda kaburini ikiwa imeiva, dunia imegawanyika  kuhusu namna ya kumkumbuka mtu kama yeye. Wanaojiita wapenda amani wanawalaumu watengeneza silaha kwa kuisababishia dunia maafa kwa kutengeneza vitu vinavyosababisha watu wasitake kukaa chini na kuzungumza.

Lakini, ukizungumza na wapigania uhuru kama wa Msumbiji na katika nchi za kiarabu, AK 47 inahusishwa na ukombozi wao. Wapo wanaomini kwamba bila ya silaha hiyo, huenda wangedumu kwenye ukoloni kwa muda mrefu.

Kama dunia ingekuwa haina silaha hata moja, huenda ingekuwa sehemu ya amani na utulivu. Lakini, wana saikolojia wanasema isingewezekana kwa dunia kuishi bila ya silaha kwa sababu mwanadamu kwa asili ni mbinafsi na angetafuta namna yoyote ya kushinda kwenye ushindani.

Pengine watu kama Kalashnikov ni sehemu ya ubinadamu wetu. Kama watu kama wao wasingekuwepo, labda dunia isingekuwa sehemu nzuri ya kuishi kuliko ilivyo sasa.

No comments:

Post a Comment