Breaking

Wednesday, January 29, 2020

SIMULIZI: NIMEKOSA NINI?: sehemu ya 3.ILIPOISHIA......
“Kumbe ndiyo huyu!” aliongea afande huyo huku akinigeukia na kuniambia,
“bwana Jerry, kuanzia sasa upo chini ya ulinzi!” Aliniambia kachero huyo ambaye uso wake ulionekana kubadilika kwa wakati huo.
SASA ENDELEA......
Hapo ndiyo nilizidi kuchanganyikiwa. Akili ikaanza kuwaza na kuwazua ni kipi nilikuwa nimefanya mpaka niwekwe chini ya ulinzi! Nikajikakamua na kuuliza,
“Ni kosa gani nililofanya afande?”
“Utaenda kuelezwa kituoni, hapa hatuwezi tukaanza kukuhoji chochote kwani tutavuruga harakati za upelelezi. Hebu mfungeni pingu haraka.” Afande huyo ambaye alikuwa anaonekana ndiyo mkubwa kicheo kuwazidi wenzake aliamru nifungwe pingu.
“Haina haja ya kunifunga pingu afande, sikimbii wala sifanyi kiburi chochote, nitaenda hivihivi.” Nilijikakamua kujitetea ili nisifungwe pingu. Nilikuwa naifikiria aibu ambayo ingenitokea endapo ningetoka mle ndani nimefungwa pingu.
Kimya kimya nilishtukia shavu linawaka moto. Kilikuwa ni kibao cha afande huyo ambacho kilinifanya nione giza totoro likifuatiwa na nyota nyota. Kilikuwa ni kibao cha haja. Nilipojaribu kupeleka mikono yangu kwenye shavu nikabaini kuwa kibao hicho kilikuwa kimeacha alama.
Kipigo kile kilinifanya niinyoshe mikono mimi mwenyewe ili nifungwe pingu, sikujali tena kuaibika ama kuchekwa na umati wa watu waliokuwa wamejazana pale nje. Mmoja wa makachelo alitoa pingu na kunikaza mikononi.
Wakati nafungwa pingu askari aliyekuwa amenifyeka kibao alikuwa bado anabwata.
“Pumbavu kabisa, unatupangia mambo ya kufanya kama sisi ni watoto wako, huna adabu hata tone”
Alipoongea hivyo alimgeukia bosi wetu kisha akamwambia,
“Mheshimiwa, ngoja tuende nae tukafanye kazi yetu, huko lazima ataenda kunyoosha maelezo yake.” Aliongea afande huyo aliyeonekana kuwa katili ajabu.
“Hakikisheni mnambana mpaka vitu vyangu vyote vipatikane.” Naye bosi wetu alisikika akiweka msisitizo kwa maafande hao.
“Hilo wala lisikupe shaka, tena watu kama hawa ndiyo huwa tunawatafuta sana.” Alichombeza afande katili aliyekuwa ameniwasha kibao.
Aliteua baadhi ya askari akawaambia wanipeleke kituoni kisha waanze kunishughulia mpaka wahakikishe ninanyoosha maelezo. Askari hao nao walitii amri waliyokuwa wameambiwa na mkuu wao huyo. Walinitanguliza tukaanza kutoka humo ndani, tukafika nje na kuwakuta watu ndiyo kwanza wanazidi kujazana.
Kwa jinsi nilivyokuwa nimewekwa chini ya ulinzi kila mtu aliyekuwepo pale nje alijua ya kwamba mimi ndiyo nilikuwa nimefanya ujambazi katika tukio hilo. Aibu niliyoipata siku hiyo kwa kweli haiwezi kuelezeka.
Tulienda moja kwa moja mpaka kwenye tenga la watuhumiwa (yaani difenda ya polisi) liliyokuwa limeegesha pembeni. Wakati tunaenda watu walikuwa wakinikodolea macho ‘kodo kodo’ utadhani nilikuwa uchi ama nimejiharibu haja kubwa, kwa kweli tukio hili lilitia fora kati ya matukio yote yaliyokuwa yamewahi kunipata katika maisha yangu.
Sikuwa na jinsi zaidi ya kujifanya siwaoni watu wote hao. Ingawa wengine walikuwa wananifahamu na wengine walikuwa hawanifahamu. Waliokuwa wananifahamu walishangaa sana kuona ninahusishwa na tukio la ujambazi, walikuwa wakiijua tabia yangu na mwenendo wangu hivyo ilikuwa ni halali yao kutoamini kwa kile kilichokuwa kikiendelea.
Siyo wao tu waliokuwa wakishangaa, hata mimi pia nilikuwa nimeshangazwa sana na kitendo cha kuanza kuhusishwa na ujambazi wakati kazi hiyo nilikuwa siifikirii kabisa kuja kuifanya japo kwa kujaribu katika maisha yangu.
Akili yangu ilipata shughuli pevu kujaribu kutafakari ni ni vigezo vipi vimetumika katika kunihusisha na hicho kitendo cha kufanya uvamizi katika ofisi yenu. Nilikuwa nikishangaa sana kuona hata bosi wangu kacharuka wakati alikuwa ananiamini kwa kiasi kikubwa kutokana na utendaji wangu mzuri wa kazi.
Tenga la polisi lilianza kuondoka eneo hilo kuelekea kituoni. Tukiwa njiani mawazo yangu yalihamia kwa mke wangu na mwanangu niliokuwa nimewaacha nyumbani siku hiyo asubuhi kwa kuwabusu mabusu motomoto. Nikaanza kujiuliza sijui mke wangu atakuwa katika hali gani, nikawa sipati picha atakavyolia pale atakapopata taarifa ya kwamba nipo mikononi mwa polisi.
‘Najua mama Chris huko patakuwa hapatoshi, na hivi ni mtu wa kulialia; atalia sana mke wangu.’ Nilijisemea kimoyomoyo huku difenda ya polisi ikizidi kutimua vumbi.
Mawazo hayo yalinifanya nichukue uamuzi wa kumtwangia simu ili nimjulishe kabisa kilichokuwa kimenisibu. Nilipeleka mkono wangu kwa shida kwenye mfuko wangu wa suruali maana nilikuwa nimefungwa pingu; nilitoa simu yangu na kuanza kubofya bofya kuitafuta namba ya mke wangu. Askari wale walikuwa wameniangalia tu huku wakiwa hawaongei chochote.
Nilipoipata namba ya mke wangu niliipiga nayo ikaanza kuita. Hakuchelewa sana kupokea,
“Halloo mume wangu mpendwa, unaendeleaje na kazi?” Alihoji mama Chris huku akionyesha bashasha kama ilivyokuwa kawaida yake akiwa anaongea na mimi.
Kabla sijamjibu nilishtukia napokonywa simu mkononi huku nikishushiwa kibao cha haja shavuni. Lilikuwa ni shavu lilelile lililopigwa pale mwanzo kule ofisini, maumivu makali yalinipata mpaka nikajikuta naropoka,
“Jamani, mbona mnanionea hivi?”
“Pumbavu usiye na haya, nani kakuruhusu kuongea na simu?” Aliunguruma mmoja wa maaskari ambaye alikuwa kaninyang’anya simu yangu.
“Japo ni mtuhumiwa lakini nina haki zinazonilinda, sasa mnavyonipiga hivi mnakuwa hamnitendei haki hata kidogo, kule ofisini mlinipiga bila sababu lakini nikawa nimemezea tu, sasa hivi tena naongea na mke wangu mnanipiga, iko wapi haki ya mtuhumiwa iliyoandikwa katika katiba ya nchi?” Nilijikakamua kudai haki yangu kwa polisi hao.
“Una haki gani jambazi sugu kama wewe? Unajifanya unaijua sana sheria kuliko sisi eeh! Ukiendelea kujifanya Karama katika nchi ya Kusadikika utaumia, sisi ndiyo tulioshikilia mpini hivyo kwa wewe uliyekumbatia makali unatakiwa kufyata mkia, mburukenge mkubwa!” Aliendelea kubwata afande huyo aliyekuwa kashikilia simu yangu.
Kumbe wakati tunaongea simu ilikuwa haijakatwa, maneno yote mke wangu aliweza kuyasikia kupitia sipika za simu yake. Ndipo nilipomuona afande huyo akibofya kitufe cha kukatia simu. Hajakaa sawa simu ilianza kuita,
“Nani huyo anampigia?” Aliuliza afande mwingine aliyekuwa kanichalaza kofi wakati najaribu kumtaarifu mke wangu kisanga kilichokuwa kimenisibu.
“Sijui ni nani, ngoja tumuulize mwenyewe.” Aliongea afande aliyekuwa ameishikilia simu yangu kisha akaunyosha mkono wake kunionyesha kwenye skrini ya simu ili niangalie nani aliyekuwa ananipigia.
Nilipotupia jicho kwenye skrini hiyo niliiona namba ya mke wangu niliyokua ‘nimeisevu’ kwa jina la ‘Tunda la roho yangu’,
“Ni namba ya mke wangu!” Nilimjibu.
Kimya kimya aliikata tena simu hiyo kisha akaamua kuizima kabisa.
“Bora ulivyoizima maana itaendelea kutupigia makelele tu.” Alisema askari mwingine aliyekuwa kimya tangu tuanze safari.
‘Kumbe hakuna hata mmoja mwenye moyo wa huruma hapa, wote wamepinda na wanaroho za kikatili.’ Nlijiwazia baada ya kumuona hata yule aliyekuwa kimwa muda wote anashabikia kunyimwa fursa ya kumpa taarifa mke wangu.
JE, NINI KITATOKEA WAKIFIKA KITUONI?

No comments:

Post a Comment