Breaking

Wednesday, January 29, 2020

SIMULIZI: NIMEKOSA NINI?: sehemu ya 5.


ILIPOISHIA.......
Vilevile ningekubali kuwa nimehusika katika kuiba wangetaka vitu virejeshwe, sasa ningevitoa wapi wakati nilikuwa sijashiriki katika wizi huo? Nilizidi kuchanganyikiwa.SASA ENDELEA......
“Kwa kweli dada yangu mimi sijaiba na sijahusika kwa namna yoyote ile katika uporaji wa hivyo vitu. Mimi nimefika tu hapo ofisini nikafungwa pingu na kuletwa huku bila hata kuelezwa nilichokitenda ama nilivyohusika na huo wizi.” Nilijikakamua na kueleza kama vile.
“Hapo nje walikuwepo watu wangapi?”
“Wengi tu!”
“Sasa kwa nini wasikamatwe hao japo mmoja wao lakini ukakamatwa wewe? Au ngoja nikurahisishie swali, kwenye hiyo kampuni mmeajiriwa wafanyakazi wangapi?”
“Wengi tu, ni zaidi ya kumi na tano!”
“Sasa kwa nini asiambiwe mwingine uambiwe wewetu?”
“Hata mimi sielewi kwa nini nimesingiziwa mimi wakati maskini wa Mungu sijahusika kabisa!”
“Hapo ujue kuna ushahidi ambao unatufanya tuamini kwa asilimia zote kuwa umeshiriki. Jerry, wewe ni mwanaume mtanashati hivyo usitufanye tukatumia nguvu kukuhoji juu ya jambo hili, kwanza mimi nakuhurumia na sipendi nikuone ukihangaika katika hiki chumba cha mateso, hebu rudisha hivyo vitu ili kuepusha hayo yote.” Aliongea mwanadada huyo akinibembeleza niseme kitendo ambacho nilikuwa sijakifanya.
“Mungu mmoja dada yangu mimi sijui chochote kuhusu tukio hilo.” Na mimi nilijaribu kupapatua kwa kuzidi kuongea uleukweli.
Mwanamke huyo aliinuka taratibu kisha akanisukumia kibao ambacho kilichonifanya nihisi kizunguzungu. Kilikuwa ni kibao cha tatu sasa ambacho kilikuwa kikiangukia kwenye shavu hilohilo. Sijakaa sawa akanisukumia kingine ambacho kililichangamsha hata lile shavu la upande mwingine ambalo lilikuwa halijaguswa. Nilisikilizia maumivu makali yasiyoelezeka.
Nilipomwangalia usoni mwanamke huyo tayari alikuwa kashabadilika. Alikuwa kashabadilika na kuvaa sura ya kinyama ambayo ikikukazia macho tu lazima uanze kutetemeka. Hakuwa na haiba kama niliyokuwa namuona nayo wakati akinitomasatomasa.
Mwanamke huyo alipiga hatua kadhaa mpaka mlangoni kisha akaufungua mlango na kuwaita wale wenzake. Wote watatu waliingia, saa wakawa mwanne jumla ukijumlisha na yeye.
“Hataki kuongea ukweli eeh!” Aliuliza mmoja wao.
“Anataka kutia adabu!”Aliitikia yule mwanamke.
Hapo sasa nilianza kuhisi mateso yanayofuatia ni ya kufa mtu. Nikaanza kujiuliza sijui nikubali tu kuwa nimeiba, palepale nikajikuta najipinga mwenyewe kuwa hata nikikubali vile vitu vilivyokuwa vimeibiwa ningevipata wapi? Kibaya zaidi nilikuwa sijaambiwa ni vitu gani vimeibiwa na thamani yake ni shilingi ngapi?
Mara mlango wa chumba hicho ukaanza kugongwa, jamaa mmoja alienda kufungua kisha mtu mmoja aliyekuwa amevaa magwanda ya kiaskari akaingia. Nilinyonga shingo yangu kuangalia ni nani aliyekuwa ameingia, hakuwa mwingine bali ni afande aliyekuwa amenitwanga kibao cha kwanza kule ofisini.
‘Mh! Limekuja tena hili limjamaa, hapa sasa shughuli imezidi kuwa pevu!’ nilijikuta nikiwaza hivyo baada ya kumuona huyo afande. Ukatili wake na sura yake ndiyo vilinifanya nianze kuwaza hivyo, alikuwa na sura mbaya na ya kutisha.
Niliweza kuwashuhudia maafande waliokuwamo humo ndani wakimpigia saluti jamaa huyo. Hapo ndiyo nikaamini kweli jamaa huyo alikuwa na cheo kikubwa kwenye jeshi hilo. Nilipoangalia vizuri kwenye gwanda lake nikaona ananyota moja begani hali ambayo ilizidi kunihakikishia kuwa jamaa alikuwa ni ‘top’
“Kashawaeleza nini huyu bwege?” Aliuliza.
“Hataki kusema ukweli, naona anatulazimisha tutumie nguvu kumhoji!” Alijibu mwanadada aliyekuwemo kwenye chumba hicho.
“Wewe nyang’au, umeficha wapi vitu ulivyoiba kwenye kampuni yenu?” Alihoji kamanda huyo. Hapo sasa niliingiwa na wasiwasi wa kuangushiwa kibao kingine muda wowote.
“Kweli kabisa afande mimi sijaiba haki ya Mungu” Nilijaribu kujitetea kwa mkuu huyu nikitegemea labda atanihurumia.
Machozi sasa yalikuwa yakinitirirka kiasi kwamba nikawa siwezi hata kuyapangusa kwani mikono yangu yote ilikuwa imefungiwa kwenye nguzo ya chuma iliyokuwa nyuma yangu. Uso wangu ulikuwa unatia huruma kwani ulikuwa umejawa na huzuni ya hali ya juu. Pamoja na hayo yote afande mwenye nyota moja wala hakunionea imani.
“Wewe ni jambazi sugu ambaye tulikuwa tunakutafuta kwa siku nyingi sana. Hivyo vitu vyote venye thamani ya milioni mia mbili umevifisha wapi? Hapa lazima urudishe na kuwataja wenzako wote unaoshirikiana nao katika kufanya uporaji.” Alizidi kuniambia afande huyo huku wenzake wote wakiwa kimya pembeni.
Kitendo cha kutajwa thamani ya vitu vilivyokuwa vimeibiwa kilinifanya niongeze kulia baada ya kuambiwa na afande huyo. Sasa nikaanza kutoa kilio cha chinichini utadhani mtoto mdogo kanyimwa pipi na mtoto mwenzake.

No comments:

Post a Comment