Breaking

Monday, February 17, 2020

Mbeya: Mtoto wa Miaka 17 Auawa Baada ya Kujaribu Kupora fedha

Mtoto Victor Mwasoro (17), ameuawa na wananchi wenye hasira kali baada ya kuvamia kibanda cha kutuma na kupokea fedha akiwa na bastola ya baba yake kwa lengo la kupora fedha.

Tukio hilo lilitokea mwishoni mwa wiki katika eneo la Sae jijini Mbeya na kwamba mtoto huyo alifariki kutokana na kipigo kikali alichokipokea.

Akielezea tukio hilo, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mbeya, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi, Ulrich Matei, alisema mtoto huyo alivamia kibanda cha Sauda Danda akiwa na bastola yenye namba za usajili 00098503 ikiwa na risasi saba.

Alisema baada ya wananchi kumshtukia walimvamia na kuanza kumshushia kipigo kwa kutumia silaha za jadi.

“Uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa mtoto huyo aliichukua silaha hiyo nyumbani kwao na inamilikiwa na baba yake, wakati anaingia kwenye kibanda hicho kujaribu kuitumia kupora alikuwa ameihifadhi kwenye kifungashio,” alisema Kamanda Matei na kuongeza:

“Baada ya kuokolewa mikononi mwa wananchi waliokuwa wanampiga alikimbizwa katika Hospitali ya Kanda ya Rufani ya Mbeya ambapo alifariki akiwa anaendelea kupatiwa matibabu.”

Kufuatia tukio hilo, Kamanda Matei aliwataka wamiliki wa silaha mkoani humo kufuata sheria za umiliki wa silaha ili zisiingie kwenye mikono ya wahalifu.

Aidha, aliwatahadharisha majambazi wanaotumia silaha kuwa kwa sasa Mkoa wa Mbeya siyo wa kujaribu kufanya matukio ya aina hiyo kwa kuwa jeshi hilo liko makini na liko tayari kukabiliana nao wakati wowote.

No comments:

Post a Comment