Breaking

Sunday, February 2, 2020

SIMULIZI: NIMEKOSA NINI?: sehemu ya 6.ILIPOISHIA.......
Kitendo cha kutajwa thamani ya vitu vilivyokuwa vimeibiwa kilinifanya niongeze kulia baada ya kuambiwa na afande huyo. Sasa nikaanza kutoa kilio cha chinichini utadhani mtoto mdogo kanyimwa pipi na mtoto mwenzake.
SASA ENDELEA.......
“Unajiliza nini, unafikiri sisi tunadanganyika kirahisi, tunajua ndiyo zenu kukataa hata kama mmeiba kweli. Pamoja na kujilizaliza kwako lazima utanyoosha tu maelezo yako leo. Afande Lulu, hebu fanyeni kazi yenu mpaka mhakikishe anasema walipovificha hivyo vitu, pia awataje na wenzake wote alioshiriki nao katika huo wizi, ni wizi mkubwa sana ambao jeshi la polisi haliwezi kuufumbia macho.” Alibwata afande huyo kisha akatoka kwenye chumba hicho.
Sasa mle ndani nilibaki na hivyo vichwa vinne vilivyokuwa vimenipokea. Jamaa mmoja kati yao akanisogelea na kuniambia,
“Tunakupa nafasi ya mwisho ya kusema kwa hiyari, kama utaendelea kukataa basi tutaanza kukushughulikia, mmeficha wapi vile vitu na wenzako ni kina nani?”
Maswali hayo yalikuwa magumu sana kuyajibu japo jibu nilikuwa nalijua. Tena mara hii hali lizidi kuwa ngumu zaidi maana tayari kuna swali jingingine lilikuwa limeshaongezeka. Hata kama ningesema nikubali tu kwamba nimeiba ili yaishe nisiteswe, swali la pili ningelijibu vipi wakati nilikuwa sijaiba? Hao wenzangu niliokuwa naambiwa nimeshirikiana nao ningewataja kina nani? Kichwa kilizidi kuuma.
“Jamani, kama kunitesa mtanitesa bure tu, lakini mimi sijaiba na sijui ki...” Nilinyamazishwa kwa bonge la ngumi ya tumbo, tumboni pakawa pamevurugika kabisa. Ilikuwa ni ngumi ya huyo jamaa aliyekuwa ameniuliza hilo swali.
Hapo sasa kipigo kikawa kimefunguliwa, nilianza kupata ngumi, vibao na mateke ya dabodabo yakiwa na kila rangi. Hapo ndiyo nilijionea mwenyewe kuwa haki ya mwenye dhiki ipo mbinguni. Kitu kilichokuwa kinaniuma ni kupewa sulubu kwa kosa ambalo nilikuwa sijalitenda hata kidogo maskini wa Mungu.
Kipigo kilirindima kwa takribani dakika kumi hivi. Mpaka wakati huo nilikuwa hoi bin taaban. Pamoja na kulia kama mtoto mdogo, jamaa hao hawakunionea huruma hata kidogo. Kilio changu ndiyo kilizidi kuwapa mzuka wa kunishushia kipigo cha paka mwizi.
Walisitisha kunipa kipondo na kuanza kuniuliza swali lao ambalo halikuwa na jibu kwangu,
“Tuambie hivyo vitu mmevificha wapi?” Aliuliza yule mwanamke ambaye mpaka wakati huo ni yeye pekee nilikuwa nimeshalijua jina lake, yaani Lulu.
“Sina kingine cha kuwaambia zaidi ya hicho nilichosema, mtaniumiza bure jamani.” Nilijibu huku machozi na kamasi zikinitiririka kwa fujo.
Kamasi sasa zilikuwa zimeshafika mdomoni, niliinama kwenye magoti na kuzifuta kisha nikainua uso wangu. Kwa kweli kilikuwa ni kipigo ambacho sijawahi kukipata tangu kuzaliwa kwangu.
Mara mmoja wa askari waliokuwa wakinishushia kipigo alienda kwenye kabati lililokuwa ukutani akachukua ‘prize spana’ kutoka kwenye kabati hilo. Mara nikamuona anarudi na kuja kusimama mbele yangu.
Wakati amesimama hapo mbele yangu mkono wake wa kulia ulikuwa umeishikilia prize spana hiyo huku akiichezea chezea kwa kuibana na kuiachia, mdomo wake ukawa unafunguka mithili ya mdomo wa mamba.
“Si unajifanya una siri, ngoja sasa tukunyooshe!” Aliongea jamaa huyo huku akizidi kunisogelea.
Mara aliinama na kunibana ngozi yangu maeneo ya mbavuni kwa kutumia prize spana yake hiyo. Alianza kubana kidogo kidogo huku akiniuliza maswali yaleyale ambayo nilikuwa nimeshawajibu lakini hawataki kulikubali jibu langu.
Huku prize spana ikiwa imeshika sawasawa kwenye ngozi yangu, jamaa huyo bila hata ya huruma alizidi kuibana. Maumivu makali niliendelea kuyasikia, nikazidi kuangua kilio lakini hakikunisaidia.
Jamaa aliendelea kunibana mpaka damu ikaanza kutoka. Sikuwa na jinsi zaidi ya kujililia huku nikiugulia maumivu. Ilifikia kipindi uzalendo ukawa umenishinda, akili yangu ikawa imevurugika kisha ustaarabu nikauweka pembeni na kuanza kuwatukana.
Nilianza kuropoka maneno ya hapa na pale huku nikiwatukana matusi ya nguoni ya kila aina unayoyafahamu ndugu msomaji. Kitendo hicho kiliwafanya wapandishe hasira zaidi ya hapo, wote wakaanza kunichangia kwa kunipiga kila mmoja alivyojisikia.
Ndani ya dakika tano walikuwa wameshanichakaza, damu zilikuwa zinanitoka sehemu mbalimbali za mwili wangu. Pamoja na kipigo hicho lakini niliendelea kuwatukana kama watoto wadogo, mishipa ya uwoga sasa ilikuwa imeshakatika, akili ilivyonituma kuropoka basi niliropoka.
Maafande hao nilianza kuwaita majina lukuki kwa wakati huo, wauaji, majambazi, mashetani na majina mengine mengi mabaya mabaya. Maneno hayo yalizidi kuwapandishia mzuka wa kunipiga, mara nilianza kuhisi kuishiwa nguvu huku macho yangu yakipoteza uwezo wa kuona, mara giza totoro lilitanda machoni kwangu na hatimaye nikawa sijitambui kabisa. Fahamu zilipotea na sikuelewa tena kilichokuwa kikiendelea kwenye kile chumba.
*****************************
NINI KITATOKEA? USIKOSE SEHEMU YA 7
PIA USISAHAU KU-LIKE, KU-SHARE NA KUTUPIA COMMENTS ZENU. PAMOJA SANA.

No comments:

Post a Comment