Breaking

Monday, February 10, 2020

Ukimapata Mchumba mwenye sifa hizi usimwache aendeMahusiano yoyote mazuri yanatengenezwa. Yana hatua za kupita. Hauamki tu asubuhi ukawa na uhusiano mzuri, ni lazima ukubali kujifunza na kufanya maamuzi sahihi ili uweze kufikia malengo yako katika muda muafaka.

Wengi wamejikuta wakipoteza muda kwa kushindwa kufanya maamuzi sahihi. Wamejikuta wakiingia kwenye uhusiano bila kujua wanataka nini na matokeo yake kujikuta wakipoteza muda na uhusiano wao unakuwa hauna malengo.

Tunafahamu kwa pamoja kwamba, ili ufikie kwenye hatua ya ndoa ni lazima upitie hatua mbalimbali. Urafiki, uchumba na hatimaye muingie kwenye hatua ya ndoa. Ukikosea kwenye moja ya hatua hizo lazima upate madhara mbele ya safari. Mchumba mzuri ana sifa gani? Utamjuaje? Hili ndiyo darasa la leo na hapa chini utakwenda kupata elimu, twende sambamba.

Mchumba mzuri ni yule ambaye tangu awali anaonesha kujitambua, anajua nini anapaswa kufanya kwa wakati muafaka. Aina au mfumo wa maisha yake unauona kabisa tangu mwanzoni kwamba huyu amekomaa kiakili, anayatamani maisha ya baadaye, anahitaji kukuza uhusiano ufikie kwenye hatua ya ndoa.

Nasema hivi kwa sababu gani, kuna baadhi ya watu ambao wanaweza kuwa na umri mkubwa lakini wanakuwa hawajitambui. Bado wanafikiri kwamba wanao muda wa kuchezea, muda wa kula ujana na hawakubali kupitwa na kila aina ya starehe.

Wao wanakwenda tu kama gari bovu. Kukicha ratiba zake zinaenda tu bila kujua zitaishia wapi. Anaanzisha mahusiano mapya kila kukicha bila kujali.

Mchumba wa namna hiyo hafai. Mchumba ambaye yeye kila uchwao anawaza starehe anawaza kutapanya mali bila kuwa na akili hata ya kuzitafuta au kuanzisha miradi ya kuzalisha zaidi huyo siyo mchumba mzuri, unaweza kumuepuka mapema.

Ndugu zangu, mchumba mzuri anaridhika na hali uliyonayo. Kwamba kwa hatua aliyofikia, anaheshimu uhusiano wake kwa kutulia na wewe na kukupa kipaumbele. Akili yake haiyumbishwi na wanawake au wanaume wazuri zaidi ya mtu wake.

Hata ikitokea ameanguka kwa mwanamke au mwanamke tofauti na mtu wake, bado akili yake itamheshimu mtu wake ambaye ndiye anampa nafasi kubwa ya kufanya naye maisha. Anamheshimu, anamthamini na anampa kipaumbele kwa namna yoyote ile.

Mchumba mzuri anawaza mafanikio. Anayazungumza mara kwa mara pindi mnapokuwa pamoja. Anakushirikisha mipango mbalimbali ya kusogea mbele katika suala zima la uhusiano wenu. Mathalan atakueleza juu ya wakati ambao anaona utakuwa ni muafaka wa kuingia kwenye ndoa.

Anapozungumza hivyo unamuona anamaanisha kutokana na jinsi siku zinavyozidi kwenda ndivyo ambavyo anajidhatiti katika kufanikisha hatua hizo muhimu katika uhusiano wenu. Unamuona namna ambavyo anajipanga, namna ambavyo anatekeleza na jinsi anavyokuhimiza mfanye mambo ya msingi ya kuwafikisha kwenye hatua hiyo.

Anaweka mipango ya kujiwekea akiba, anajikita zaidi katika kubana matumizi na kuwekeza kwenye miradi. Anakushauri na wewe ujikite kwenye miradi maana anahitaji muunganishe nguvu ili muweze kuyafikia haraka mafanikio.

Mchumba mzuri anakuwa na hofu ya Mungu. Anaamini kwamba Mungu pekee ndiye muweza wa yote. Anakushauri na wewe kuishi katika kumtegemea Mungu. Anakushauri juu ya hatua za kupita ili muweze kuifikia hatua hiyo muhimu.


No comments:

Post a Comment