Breaking

Sunday, March 22, 2020

KIFO: Familia ya Marealle wapelekana kortini mazishi ya mama yao


By Daniel Mjema, Mwananchi dmjema@mwananchi.co.tz
Moshi. Mfanyabiashara anayemiliki vitega uchumi mbalimbali ndani na nje ya mkoa Kilimanjaro, Frank Marealle amefungua shauri mahakamani akipinga bibi wa miaka 105 kuzikwa eneo analodai ni lake.

Mwanamke huyo, Veronica Mlang’a (pichani) ni mke wa mwisho wa Mangi David Mlang’a na ni mama mdogo wa mfanyabiashara huyo, ndiye pekee aliyekuwa amebakia miongoni mwa wake sita wa marehemu Mlang’a Marealle.

Mangi David alipokea umangi kutoka kwa mangi mkuu Marealle wa kwanza mwaka 1916, akafariki mwaka 1962 na mangi huyo alikuwa na wake sita, Veronica ndio akiwa wa sita.

Katika maombi yake namba 76/2020 aliyoyawasilisha Baraza la Ardhi na Nyumba Moshi, Frank anadai ni mmiliki halali wa eneo hilo na aliidhinishwa na kijiji cha Lyamrakana Marangu Aprili 29, 2015.

“Mama yangu alikuwa wa kwanza kuishi hapo tangu enzi ardhi hiyo ikiwa haijakaliwa na mtu na watoto wake wote nikiwamo mimi tulizaliwa na kukulia eneo hilo hadi leo,” anaeleza Marealle.

Marealle ambaye pia ni mangi wa Wachagga wa Marangu, amefungua shauri hilo dhidi ya mtoto wa bibi huyo, Acley Mlang’a Marealle, akidai mtoto huyo ana nia ya kumzika mama yake eneo hilo.

Kupitia kwa wakili wake Modestus Njau, Marealle anaeleza kuwa maombi hayo ni ya dharura kwa kuwa Veronica aliyefariki Machi 14, anatarajiwa kuzikwa eneo hilo wakati wowote.

Hivyo, mfanyabiashara huyo anaomba maombi hayo yasikilizwe chemba na mahakama itoe amri ya kumzuia mjibu maombi (Acley) na ndugu zake au mawakala wake, kuendelea na maandalizi ya mazishi eneo hilo.

Acley alipotafutwa na jana alikiri kufahamu uwapo wa kesi hiyo, akasema wataendelea na mazishi kama kawaida leo kwa kuwa hakuna amri yoyote iliyotolewa na Mahakama.

“Hatuna amri yoyote ya mahakama kutuzuia tusimzike hapo kwa hiyo tutampumzisha mama yetu hapo kama alivyoacha wosia hilo eneo alishamrithisha mjukuu wake anaitwa Joseph,” alisema

Wosia

Wosia wa marehemu alioutoa Aprili 4, 2015 ambao gazeti hili lina nakala yake, unaeleza kuwa alimrithisha mjukuu wake huyo shamba hilo lenye ukumbwa wa heka mbili aliloachiwa na mumewe.

Mwananchi

HIZI HABARI ZA HIVI ZINAPATIKANA GODSTAR ONLINE >>BONYEZA HAPA KUDOWNLOAD APP YA GODSTAR ONLINE

No comments:

Post a Comment