Breaking

Saturday, March 14, 2020

Mahakama yamaliza Utata Mchungaji Msigwa Kulipiwa Faini na Magufuli


By Hadija Jumanne, Mwananchi hjumanne@mwananchi.co.tz
Dar es Salaam. Baada ya Rais John Magufuli kumlipia faini ya Sh38 milioni, mbunge wa Iringa Mjini, mchungaji Peter Msigwa, Chadema waliomba fedha zilizolipwa benki kwa ajili ya mbunge huyo zitumike kumlipia faini mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche.

Msigwa na viongozi wengine wa Chadema wakiongozwa na mwenyekiti wa Taifa, Freeman Mbowe, waliamriwa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kulipa faini baada ya kuwatia hatiani kwa makosa ya kufanya mkusanyiko na maandamano yasiyo halali na uchochezi.

Juzi Rais Magufuli alimlipia Msigwa faini ya Sh38 milioni kati ya Sh40 milioni alizotakiwa kulipa mbunge huyo ili atoke jela baada ya familia yake kuchangishana Sh2 milioni. Hata hivyo, malipo kwa mchungaji Msigwa, yaliibua mjadala baada ya kutolewa taarifa mbili tofauti kuhusu kumlipia faini .

Taarifa hizo mbili ziliibua utata, huku watu wakihoji ilikuwaje mbunge huyo akalipiwa faini mbili tofauti, wakati namba ya malipo ya pesa hizo (control number) kutoka mahakamani kwa kawaida huwa ni moja tu kwa kila mtu anayetaka kufanya malipo.

Jana, Mahakama ya Kisutu ilitoa ufafanuzi wa mkanganyiko huo, ikibainisha kuwa malipo yaliyoanza kuwasilishwa mahakamani hapo ni ya Rais Magufuli.

Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Kisutu, Godfrey Isaya aliliambia Mwananchi kuwa namba ya malipo ya faini ya mtu aliyehukumiwa kulipa faini, huweza kutolewa kwa watu zaidi ya mmoja na kwamba hilo si tatizo. Alisema namba ya malipo, inakubali malipo kama kawaida na huingia katika mfumo ambao unaweza kutambulika na hata kama mtu akifanya kosa lingine akahukumiwa, akilipa faini atapewa ‘control namba’ hiyo hiyo kulipia.

Alifafanua kuwa malipo hayo huingizwa kwenye mfumo wa kumbukumbu za mahakama baada ya mlipaji kuwasilisha risiti ya benki ya malipo husika.

“Kwa hiyo malipo yaliyoingia kwanza kwenye`system’ ni ya Rais Magufuli na sisi hayo ndiyo tuliyoyapokea na kuyaidhinisha,” alisema Hakimu Isaya.

Alisema kutokana na hali hiyo, uongozi wa Chadema uliwasilisha maombi mahakamani hapo ili malipo waliyolipa kwa Mchungaji Msigwa yahamishiwe kwa Heche. Alisema kuwa maombi hayo ya kubadilisha malipo yaliwasilishwa mahakamani hapo na mwanachama wa Chadema, Evans Luvinga kwa niaba ya chama hicho na kwamba yeye aliona maombi hayo jana.

“Hivyo na sisi kama mahakama tumekubaliana na maombi hayo na taratibu hizo zimeshafanyika,” alisema Hakimu Isaya.

Ofisa habari wa Chadema, Tumaini Makene akizungumza na Mwananchi jana alikiri chama hicho kuwasilisha ombi la kuhamishwa kwa fedha hizo. Kuhusu nani aliyetangulia kufanya malipo, Makene alisema Chadema walichukua namba za malipo siku ya pili baada ya hukumu na kufanya malipo mapema juzi.

Ilivyokuwa awali

Taarifa zilizozua mkanganyiko ni zile zilizotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Gerson Msigwa pamoja na kaka wa Msigwa, Benert Msigwa ikieleza kuwa Rais John Magufuli alichangia kiasi cha Sh38 milioni kati ya Sh40 milioni alizotakiwa kulipa.

Wakiwa mahakamani Kisutu baada ya kuwasilisha risiti ya malipo hayo benki kwa ajili ya kupata kibali cha mahakama cha kumtoa gerezani, waliwaeleza waandishi wa habari kuwa uamuzi huo wa Rais Magufuli ulitokana na maombi ya familia hiyo, yakiongozwa na kaka wa Mchungaji Msigwa.

Msigwa wa Ikulu alisema familia ya Mchungaji Msigwa baada ya kuchangishana walifanikiwa kupata Sh2 milioni tu na hivyo kuwa na upungufu wa Sh38 milioni na ndipo walipoamua kwenda kumuomba Rais Magufuli awasaidie kupata kiasi kilichobaki kwakuwa wana undugu naye.

Hata hivyo muda mfupi baada ya taarifa za Rais Magufuli kumlipia Mchungaji Msigwa kutolewa, uongozi wa Chadema nao ulitoa taarifa kwamba tayari walikuwa wameshamlipia mbunge huyo faini ya Sh40 milioni. Chadema walisambaza mitandaoni risiti ya malipo hayo benki.

Msigwa na viongozi wengine nane wa chama hicho walihukumiwa faini hiyo baada ya kupatikana na hatia katika mashtaka 12 kati ya 13 yaliyokuwa yakiwakabili katika kesi ya jinai namba 112 ya mwaka 2018.

Washtakiwa wengine katika kesi hiyo walikuwa ni mbunge wa Tarime mjini, Ester Matiko; Mbunge wa Kawe, Halima Mdee; mbunge wa Kibamba, John Mnyika, Salum Mwalimu, naibu katibu mkuu Chadmea Zanzibar na aliyekuwa katibu mkuu wa chama hicho, Dk Vicent Mashinji aliyehamia Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Walikuwa wakidaiwa kutenda makossa hayo wakati wa mkutano wa kufunga kampeni za uchaguzi mgodo wa jimbo la Kinondoni, Februari 16,2018, katika viwanja vya Buibui, Mwanyamala na katika barabara ya Kawawa jijini Dar es Salaam.

Machi 10, mahakama hiyo katika hukumu iliyotolewa na Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba aliyekuwa akiisikiliza kesi hiyo iliwatia hatiani kwa mashtaka 12 kati ya 13 baada ya kuwaachia huru wote katika shtaka la kwanza kula njama kutenda makosa.

Hivyo hivyo iliwamuru kulipa kila mmoja kulingana na makosa yaliyokuwa yakimkabili.

Mbowe aliamuriwa kulipa faini ya jumla ya Sh70 milioni, baada ya kupatikana na hatia katika mashtaka 8; Msigwa, Mdee, Heche na Bula kila mmoja Sh40 milioni kwa mashtaka manne kila mmoja na Mnyika, Mwalimu, Matiko na Mashinji Sh30 milioni kwa mashtaka matatu kila mmoja.

HIZI HABARI ZA HIVI ZINAPATIKANA GODSTAR ONLINE >>BONYEZA HAPA KUDOWNLOAD APP YA GODSTAR ONLINE

No comments:

Post a Comment