Breaking

Wednesday, March 11, 2020

Mama Kanumba Amsamehe Baba Kanumba


MUNGU mkubwa! Ndivyo unavyoweza kusema kutokana na ule ugomvi uliodumu kwa miaka 8 kati ya wazazi wa aliyekuwa staa wa filamu Bongo, marehemu Steven Charles Kanumba, kuisha ikiwa ni baada ya mama, Flora Mtegoa kumsamehe mzazi mwenzake, Charles Kanumba.

Mama Kanumba alitangaza kumsamehe mzazi mwenzake huyo kwenye kipindi cha Kata Mbuga kinachorushwa na +255 Global Radio, ikiwa ni baada ya kukutanishwa ghafla na kaka wa Kanumba (wa mama mwingine), Mjanael Kanumba ambaye alifika Dar kwa ajili ya kushughulikia fedha za Kanumba alizofanya kazi na kampuni mbalimbali akiwa amemuwakilisha baba yake.

ILIKUWAJE?

Kutokana na kuwepo kwa mgogoro wa muda mrefu ambao pia umeongezeka kutokana na mirathi ya Kanumba, +255 Global Radio iliamua kuingia kazini ambapo ilimualika kila mmoja kwa muda wake. Hakuna aliyejua kama atakutana na mwenziye, yaani mama Kanumba na kaka wa Kanumba.

Ndani ya studio alitangulia kuingia mama Kanumba kisha Mchungaji Daudi Mashimo, baada ya hapo akaingia Kaka wa Kanumba, hivyo kumfanya mama Kanumba kutokwa na kijasho chembamba.

MAMA KANUMBA APANIKI

Mara baada ya kijana huyo kuingia studio, mama Kanumba alionesha kukasirika na kutaka kuondoka huku akitokwa jasho na kupata kiu ghafla, ambapo kwa busara za Mchungaji Daud Mashimo na watangazaji, walifanikiwa kumtuliza na kukaa.

Baada ya mama Kanumba kutulia, kila mmoja alitoa dukuduku lake na baada ya saa mbili kupita, kila kitu kilikuwa sawa.

MAMA KANUMBA ASAMEHE

“Unajua nimekaa na kinyongo miaka nane sasa, lakini ilifika wakati ikabidi nisamehe. Nilikwenda kupiga magoti kanisani mbele ya madhabahu na kusamehe kila kitu, nikamuachia Mungu ashughulike na wabaya wangu.

“Niseme tu kwamba, nimemsamehe mzazi mwenzangu na nampenda sana baby wangu, ila kwa kuwa amekuja mwanaye kwa niaba yake, basi naomba amfikishie hizi taarifa na amwambie na yeye aende kanisani akatubu kweli dhambi zake zote”, alisema.

KAKA WA KANUMBA SASA

“Naishukuru +255 Global Radio kwa hili mlilolifanya kwetu, ni jambo zuri sana sikutegemea, namuomba tena msamaha mama yangu (mama Kanumba) kwa yote yaliyotokea kwenye familia, nampenda na kumheshimu sana na nitaendelea kufanya hivyo siku zote, naamini hata siku akikutana na baba mambo yatakuwa safi,” alisema.

NENO LA MCHUNGAJI

Kwa upande wa mchungaji aliyewapatanisha, Mashimo alimalizia kwa kusema;

“Hili ni jambo kubwa na la nidhamu sana, huyu mama ukimuangalia anaonekana amesamehe kweli kutoka moyoni, naomba sasa mkaishi vizuri na mshirikiane kwa kila jambo na Mungu akazidi kuwabariki.”

KUTOKA KWA WIKIENDA

Mama Kanumba hongera kwa kusamehe, jambo ulilolifanya ni jema maana umekuwa na moyo wa kusamehe kwa kuwa binadamu sisi siyo kitu, maisha ni mafupi mno, hakuna faida ya kuwa na vinyongo.

Kwa upande mwingine tunaamini mtaenda kumaliza vyema hata lile suala la mgawanyo wa fedha za kazi alizozifanya marehemu Kanumba enzi za uhai wake, hakutakuwa na mvutano tena kama ilivyokuwa mwanzo.

STORI: DULLY FLEX, DAR

HIZI HABARI ZA HIVI ZINAPATIKANA GODSTAR ONLINE >>BONYEZA HAPA KUDOWNLOAD APP YA GODSTAR ONLINE


No comments:

Post a Comment