Breaking

Sunday, March 8, 2020

Mbatia: Sijatumwa na Magufuli kuiangusha Chadema Mbeya


By Hawa Mathias, Mwananchi hmathias@mwananchi.co.tz
Mbeya. Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia amesema mazungumzo yake na Rais wa Tanzania, John Magufuli ya Machi 3, 2020 Ikulu jijini Dar es Salaam hayakulenga kukiangusha Chadema katika majimbo ya Rungwe, Busokelo na Kyela katika uchaguzi mkuu wa Oktoba, mwaka huu.

"Nimekuja Mbeya kwenye ziara ya kukiimarisha chama cha NCCR si kwamba nimetumwa na Rais John Magufuli kuja kukiua Chadema. Hiyo ni hofu yao, majungu na ufike wakati kujenga hoja za fikra,” amesema Mbatia leo Jumamosi Machi 7, 2020 katika mkutano na waandishi wa habari mjini Mbeya.

Amebainisha kuwa ziara yake mkoani humo ni kwa ajili ya kukiimarisha chama na kuangalia changamoto zinazowakabili wananchi katika majimbo hayo.

Machi 3, 2020 katika kinachoweza kutafsiriwa kuwa ni kuibua matumaini mapya ya maridhiano, Rais Magufuli alikutana na kufanya mazungumzo na viongozi watatu wa vyama vya upinzani Ikulu, Dar es Salaam.

Mazungumzo hayo yalijikita katika masuala ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 na kuhimiza haja ya kudumisha amani, usalama na upendo.

Viongozi waliokutana na Rais kwa nyakati tofauti ni mshauri mkuu wa Chama cha ACT-Wazalendo,  Maalim Seif Sharif Hamad;  Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahimu Lipumba na Mbatia.


Hata hivyo, haikueleweka mara moja kama kukutana huko kutakuwa na mwendelezo wa vikao vingine vya viongozi wengine wa upinzani.

Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Gerson Msigwa alipoulizwa kwa simu alisema suala hilo ni siri ya ratiba za rais.

Baada ya asubuhi viongozi hao kukutana na Rais, mchana Mbatia alikutana na waandishi wa habari na kumpokea katibu mwenezi wa zamani wa Baraza la Vijana Chadema (Bavicha), Edward Simbeye  na kisha kutangaza kuanza ziara ya kukiimarisha chama hicho.

Katika mkutano wa leo, Mbatia amesema, “nimefanya ziara katika jimbo la Rungwe, Busokelo na Kyela kimsingi nimejionea hali halisi barabara mbovu, uchafu na kwetu sisi kama NCCR tunataka kusimamisha wagombea katika nafasi zote za udiwani, ubunge na urais ili kujenga utu, ujamaa na umoja wa Watanzania.”

Mbatia amesema vyama vya siasa  nchini vinajidanganya kama ni bora kuliko vyama vingine na kwamba hakuna chama wala serikali yenye nchi, “bali kila chama kina haki ya kushika dola  na kuongoza wananchi na ndio maana mwalimu Nyerere (Julius) aliingiza mfumo wa vyama vingi ambavyo vinapaswa kushindana na hoja na si matusi, kejeli na propaganda zisizo na maslahi mapana kwa Watanzania.”

HIZI HABARI ZA HIVI ZINAPATIKANA GODSTAR ONLINE >>BONYEZA HAPA KUDOWNLOAD APP YA GODSTAR ONLINE

No comments:

Post a Comment