Breaking

Friday, March 27, 2020

Shamim na mumewe kusomewa maelezo ya mashahidi

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu inatarajia kuwasomea maelezo ya mashahidi na vielelezo mfanyabiashara, Abdul Nsembo maarufu kama Abdulkandida (45) na mkewe Shamim Mwasha (41) Mosi Aprili 2020. 

Washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka ya kusafirisha dawa za kulevya aina ya Heroin Hydrochloride zenye uzito wa gramu 232.70 ambapo watasomewa maelezo ya mashahidi na vielelezo hivyo katika mahakama hiyo. 

Wakili wa Serikali, Wankyo Simon akidai hayo leo Machi 27, 2020 mbele ya Hakimu Mkazi, Rashid Chaungu alidai kuwa wamepewa taarifa kwamba  maelezo ya mashahidi na vielelezo vimewasilishwa katika mahakama hiyo. 

"Shauri lilikuja kwa ajili ya kutajwa na tumepata taarifa tayari maelezo ya mashahidi na vielelezo vimeshawasilishwa na lipo upande wetu hivyo tunaiomba mahakama hii ipange tarehe nyingine ya karibu ya kuwasomea kwa kuwa Hakimu anayeendesha shauri hili hayupo," amesema Simon. 

Baada ya maelezo hayo Hakimu Chaungu aliahirisha shauri hilo hadi Mosi Aprili 2020 itakapokuja kwa ajili ya kuwasomea maelezo ya mashahidi na vielelezo.


HIZI HABARI ZA HIVI ZINAPATIKANA GODSTAR ONLINE >>BONYEZA HAPA KUDOWNLOAD APP YA GODSTAR ONLINE

No comments:

Post a Comment