Breaking

Wednesday, March 11, 2020

Vita Nzito na Mondi… Zari, Tanasha Waungana


MWANAMUZIKI wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ au ‘Mondi’ si ameimba katika wimbo wake uitwao Baba Lao; ‘hata wakiungana… aah wapi’ sasa Tanasha Donna na Zarinah Hassan ‘Zari’ wameungana katika vita dhidi yake ambayo haina jina, IJUMAA WIKIENDA linakupa uhondo kamili.

Zari, raia wa Uganda mwenye maskani yake, Durban nchini Afrika Kusini na Tanasha ambaye ni Mkenya, wote wamepata kuwa wapenzi wa Mondi na kufanikiwa kuzaa naye, lakini wameambulia kupigwa kibuti kwa staili inayofanana.

ZARI AUNGANA NA TANASHA

Siku chache baada ya Tanasha kutemwa katika uhusiano wa kimapenzi na Mondi, Zari ambaye alikuwa wa kwanza kabla yake kuwa na uhusiano na Mondi na kuachwa, aliibuka na ujumbe mzito aliouweka kwenye ukurasa wake wa Instagram uliodaiwa kwenda kwa Tanasha.
“Ndiyo, lazima ujue chui hawezi kubadilika madoa na haijalishi ni mara ngapi nyoka anajivua magamba, lakini anabaki kuwa nyoka!”

Ni maneno ya mwanamama Zari kwenda kwa Tanasha ambayo yaliambatana na hisia zake kuwa anaheshimu uamuzi wa Tanasha kuachana na mzazi mwenzake, Mondi.

Nyoka anayetajwa kuwa hawezi kubadilika licha ya kujivua gamba katika ujumbe huo mzito wa Zari, alitafsiriwa kuwa huwenda anamaanisha ni Mondi ambaye amekuwa na desturi ya kuzaa na wanawake tofauti kisha kuwaacha na kuanzisha uhusiano mpya wa kimapenzi.

MAJUTO YA TANASHA BAADA YA KUACHWA

Takriban mwaka mmoja uliopita, wakati uhusiano wa Mondi na Tanasha ukiwa hoti, Zari ambaye wakati huo alikuwa akiugulia majeraha ya kuachwa kiaina na alimuonya Tanasha kuwa awe makini na mwanaume huyo ambaye yeye alimuita kuwa ni mtu anayechezea hisia za wanawake.

Siku chache baada ya habari ya mjini kuwa ni kuvunjika kwa penzi la Tanasha na Mondi, mwanadada huyo aliandika katika ukurasa wake wa Instagram maneno yaliyosomeka kuwa yuko ‘singo’.

Hata hivyo, baadhi ya mashabiki wa Tanasha nchini Kenya kupitia kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii, wamekuwa wakimlaumu mwanamke huyo kwamba, hakuwa makini alipoonywa kutojiachia kimapenzi na Mondi.

Chanzo kilicho karibu na Tanasha kilimjibu mmoja kati ya mashabiki hao; ‘kidonda hakipakwi chumvi’ kuonesha kuwa Tanasha naye anaugulia maumivu ya kuachwa.


ZARI AZIDI KUTOA POVU

Pengine akionesha kukerwa na kitendo alichofanyiwa mwanamke mwenzake, Zari aliendelea kushusha ujumbe kwenye ukurasa wake wa Instagram ambao ulionesha kuwa yuko nyuma ya Tanasha katika wakati huu mgumu.

“Kuna mambo huwezi kuyaficha, kwa muda mrefu; jua, mbalamwezi na ukweli.”

Zari aliongeza kumshauri Tanasha kuwa ajiandae kulea mtoto aliyezaa na Mondi peke yake kama yeye anavyowalea watoto wawili aliozaa na msanii huyo nguli kutoka Bongo.

MPANGO WA MONDI KUPORWA MTOTO WA TATU WAVUJA

Vyanzo mbalimbali kutoka Kenya vililiambia Gazeti la IJUMAA WIKIENDA kuwa baadhi ya marafiki wa karibu wa Tanasha wamemshauri asikubali kumuacha mtoto wake kwenye umiliki wa baba yake.

“Ingawa mtoto wa Tanasha kazaliwa Tanzania, kwa hiyo ana uraia wa nchi hiyo, lakini zipo taarifa kutoka kwenye familia hiyo kuwa wana mpango wa kumbadilisha uraia awe Mkenya.

“Sasa sijui kama Tanasha anafuata kile alichokifanya Zari baada ya kuwapatia uraia wa Afrika Kusini watoto aliozaa na Mondi au ni akili zake tu,” kilisema chanzo kingine.

Zari ambaye amezaa na Mondi watoto wawili; Tiffah na Nillan walipoachana alilazimika kuwapa uraia wa Afrika Kusini ambako yeye anaishi na kwamba malezi yao yako chini yake.

Kwa msingi huo, huwenda Mondi akajikuta akiporwa mtoto wa tatu kibabe na Tanasha na kujikuta akisalia na mmoja aliyezaa na Mbongo mwenzake, Hamisa Mobeto.

TANASHA, ZARI KUMSHAMBULIA MONDI

Wakati hayo yakiendelea, mpango wa Tanasha na Zari kuendelea kumchafua Mondi mbele ya jamii kwamba ni mwanaume kivuruge, umevuja na kwamba hayo yatafanywa kwa lengo la kuwaonya wanawake wengine kuwa makini na msanii huyo.Mara kadhaa Zari, amekuwa akiibuka na kumtolea maneno ya kumkejeli Mondi kuwa ni mwanaume ambaye hafai kuitwa baba wa familia.

Vita hiyo ya maneno huwenda ikaendelezwa na Tanasha ambaye amewaahidi mashabiki wake kuwa atazungumza yote yaliyomsibu kupitia wimbo ambao anautaarisha.“Tanasha, sasa anakesha studio akiandaa ngoma kali zitakazoeleza kilichojiri kati yake na mzazi mwenzake huyo,” mtu wa karibu na Tanasha ameeleza kwenye mtandao mmoja wa kijamii nchini Kenya.

MONDI AONEKANA KUPUUZA

Alipotafutwa na mwandishi wetu ili azungumzie uhusiano kati yake na Tanasha kuvunjika na uwepo wa mpango wa kumchafua Mondi, alionesha kupuuza na kusema kwa ufupi;

“Kuhusu nani? Nitamzungumzia baadaye.”

Mondi amekuwa na uhusiano moto wa kimapenzi na Wema Sepetu ambaye hakufanikiwa kupata naye mtoto, hata hivyo baadaye alimtupia virago na kujitwalia mrembo Zari ambaye alikuja kupinduliwa na Hamisa kisha naye kutolewa kwenye reli na Tanasha.

HIZI HABARI ZA HIVI ZINAPATIKANA GODSTAR ONLINE >>BONYEZA HAPA KUDOWNLOAD APP YA GODSTAR ONLINE

No comments:

Post a Comment