Breaking

Monday, April 6, 2020

Baada ya Kusepa Bongo, Tanasha Aibua Mazito ya Mondi


INAWEZA ikakushangaza, lakini ukweli unabaki kuwa familia ya staa wa muziki barani Afrika kutoka nchini Tanzania, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’, inaongoza kwa matukio yenye visa na mikasa vinavyoifanya iwe maarufu zaidi katika anga la burudani.

Habari ikufikie kwamba, baada ya Wema Isaac Sepetu, Zarinah Hassan ‘Zari The Boss Lady’ na Hamisa Mobeto kulalamika juu ya familia ya Diamond au Mondi, sasa ni zamu ya Tanasha Donna.

Wote waliotajwa hapo juu ni mastaa wakubwa Afrika Mashariki ambao walipata kuwa wapenzi na wazazi wenza wa Mondi.

MARA YA KWANZA…

Kwa mara ya kwanza baada ya kuachana na Mondi, yapata mwezi mmoja uliopita, Tanasha ameshindwa kujizuia, amefuata nyayo za Wema, Zari na Mobeto, ameibua mazito juu ya jamaa huyo na mama yake mzazi, Sanura Kassim almaarufu kama Bi Sandra au Mama Dangote.

Katika mahojiano maalum na jarida kubwa la burudani barani Afrika la True Love Magazine lililoingia mtaani Aprili Mosi, wiki hii, Tanasha anamlalamikia Mama Dangote au Mama D kuwa chanzo cha kuvurugika kwa penzi lake na Mondi.

Amedai kuwa, mama Dangote amekuwa akiingilia mno uhusiano wa kimapenzi wa mwanaye huyo na kusababisha kutodumu nao.

MAMA DANGOTE ATETEWA

Hata hivyo, wakati Tanasha akitoa tuhuma hizo nzito, wapo wanaotumia nguvu kubwa kumtetea Mama Dangote kuwa hufanya hivyo kwa nia njema na upendo alionao kwa mwanaye huyo kwa kuona mpenzi aliyenaye hawezi kumfikisha kwenye mafanikio au malengo aliyojiwekea kama mwanamuziki mkubwa.

ALIYOFANYIWA NA MAMA DANGOTE

Katika mahojiano hayo, Tanasha anajaribu kuelezea yale aliyofanyiwa na Mama Dangote na kwamba ni mtu wa aina gani.

Anasema; “Kuhusu mipaka kati yake na mwanaye (Mondi) haikuwepo, Mama Dangote yupo kinyume sana na mama mkwe wa kisasa anavyotakiwa kuwa.”

Kwa mujibu wa Tanasha, uhusiano wake na baba mtoto wake, Mondi ulishindikana au kufeli kwa sababu Mama Dangote alijihusisha nao bega kwa bega; yaani Tanasha akitoa mguu naye anaweka mguu!

Anasema kuwa, awali alijitahidi kuwa mpole na kumwachia Mama Dangote kujihusisha na kila kitu katika penzi lao kwa sababu hakutaka kuonekana hana heshima hata kidogo.

MONDI MTOTO WA MAMA

Wakati hayo yakiendelea, Tanasha anasema kuwa, Mondi hakuwahi kuona kama ni tatizo kwa sababu ni ‘mtoto wa mama’.

“Kamwe hakuona umuhimu wa kumwambia mama yake amheshimu mpenzi wake,” anasema Tanasha.

MONDI UPANDE WA MAMA’KE

Kwa mujibu wa Tanasha, Mondi hakuwa upande wake hata pale ambapo kulitokea kutokuelewana kati yake na Mondi, badala yake alikuwa upande wa mama yake, pamoja na kujua kwamba, mama yake ni mkorofi.

TANASHA AKOSA MTETEZI

Matokeo yake, Tanasha anasema alijikuta amebaki peke yake bila mtetezi.w

Mahojiano hayo ya Tanasha yanaacha mshangao mkubwa juu ya kile kilichokuwa kikiendelea nyuma ya pazia la penzi lake na Mondi kwamba, kumbe mambo yalikuwa mazito, tofauti na matarajio ya wengi kwamba walikuwa ‘Paradiso’.

Hata hivyo, hii si mara ya kwanza kwa Mama Dangote kusemwa kwa namna hii.

ZARI NA BBC

Katika mahojiano yake na Shirika la Habari la Uingereza (BBC-Swahili), mara tu baada ya kumwagana na Mondi, miaka miwili iliyopita, Zari alizungumza hivihivi kama anavyozungumza Tanasha, lakini wapo walioamini kuwa alikuwa na hasira ya kuchezewa na kuishia kuzalishwa watoto wawili; Tiffah Dangote na Prince Nillan kisha akaachwa.

SASA ITAKUWAJE?

Katika mazingira ya aina hii, wananzengo wanauliza. Je, Mondi anaweza kupata mke wa kudumu naye mbele ya mama yake au sasa itakuwaje?

UKARIBU WA MONDI NA MAMA’KE

Mara kadhaa ukaribu wa Mondi na mama yake umekuwa ukiibua sintofahamu.

Mara kadhaa wameripotiwa kusafiri pamoja ndani na nje ya nchi kwenye matamsha ya jamaa huyo huku wakijiachia watakavyo kwa vituko na utani ambao ni nadra sana kuonekana katika familia za Kitanzania.

“Diamond na mama yake kwa kweli wanaishi maisha ya raha sana, kama hujaambiwa, huwezi kudhani kama ni mtu na mama yake. Wanataniana sana, wanaishi Kizungu,” alisema mmoja wa watu wa karibu wa familia ya Mondi.

MTU mwingine wa karibu na familia hiyo alilieleza gazeti hili kuwa, maisha hayo ya Mondi na mama yake yalianza muda mrefu kabla hata nyota ya jamaa huyo haijang’aa katika ulimwengu wa muziki.

“Tangu utotoni, Mondi na mama yake walikuwa wanapendana sana, angalia hata picha zao za TBT (Throwback Thursday utaratibu wa kuposti picha au matukio ya zamani kwenye mitandao ya kijamii siku ya Alhamisi), utaona picha zao za mabusu ya upendo wa mama na mtoto.

“Labda ni kwa sababu waliachwa na baba yake wakati Mondi akiwa mdogo, hivyo ana upendo wa dhati na mama yake.

“Ukweli ni kwamba, Mondi anamsikiliza zaidi mama yake kwa sababu wametoka kwenye maisha ya taabu sana na hao wanawake wamekuja tu, hawawezi kuchukua utawala kirahisi kiivyo.


“Mimi sioni ubaya kwa Mama Dangote kumsimamia mwanaye, hataki mwanaye atumbukie kwenye uhusiano ambao anaona utamtesa baadaye ndiyo maana anafanya kila liwezekanalo kuwa karibu na mwanaye, watu waache, wao ndiyo wanajua walivyoteseka na maisha yao,” alisema mtu huyo kwa ombi la kutotajwa gazetini.

NENO LA ESMA

Kwa upande wake dada wa Mondi, Esma Khan ‘Esma Platnumz’ aliwahi kulieleza gazeti hili kuwa, wawili hao (Mondi na Mama Dangote) wanaishi Kizungu, kwani huwezi kukuta mtu anakuwa na sheria kali kama zile za wazazi wa kizamani.

“Siyo wao peke yao, familia nzima tunaishi kirafiki sana, ukimkuta Mondi, mama, mimi au hata ndugu mwingine, jinsi tunavyotaniana na kucheka huwezi kuamini, siyo mambo ya kufuatiliana, ni ishu ya upendo kati yetu,” alisema Esma.

MAMA DANGOTE ANASEMAJE?

Katika mahojiano ya mara kwa mara na Magazeti Pendwa ya Global Publishers, Mama Dangote amewahi kunukuliwa akisema kuwa, kwenye familia yake wamekuwa wakiishi kama marafiki tangu kitambo na hiyo ndiyo staili ya maisha yao hata kabla Mondi hajawa maarufu.

“Tumeishi hivi tangu siku nyingi, ukitukuta nyumbani ni kama vile marafiki kumbe mtu na mama yake. Si kwa Nasibu (Mondi) tu, hata kwa watu wetu wa karibu yaani ni fulu burudani na haina maana kwamba tunamkomoa mtu yeyote,” alinukuliwa Mama Dangote.

MWISHO WA MONDI NA TANASHA?

Kuhitilafiana kwa Mondi na Tanasha kulianza kwa uvumi kwamba wapenzi hao wameachana.

Hatua hiyo ilijiri baada ya Tanasha kuposti ujumbe kwenye ukurasa wake wa Mtandao wa Instagram akiwaonya wanawake wenzake kutovumilia wapenzi ‘wanaojihusudu’.

Katika msururu wa machapisho hayo, Tanasha alitoa dalili kwamba mambo si shwari katika uhusiano wake na Mondi.

Tanasha aliandika; “Watu kama hawa hawana roho ya ubinadamu iliyosalia ndani mwao. Ushetani mtupu, ni kama kucheza dansi na shetani. Tuwasamehe, waacheni na kumwacha Mungu kukabiliana nao. Watu kama hao kila mara huamini kwamba majuto hayatawafikia hadi yanapowafikia. Mara nyingine unahitaji uzoefu ili kujifunza, ombeni kila siku mara tano kwa siku iwapo itawezekana. Kwa sababu kukabiliana na baradhuli ni sawa na kukabiliana na shetani mwenyewe. Lindeni roho zenu.”

Katika uvumi huo ilielezwa kwamba, mtangazaji huyo aliyebadilika na kuwa msanii wa muziki, alilumbana na Mama Dangote alipojaribu kuondoka Tanzania na mwanawe.

“‘Mungu huwaondoa watu fulani katika maisha yako kwa sababu alisikia mazungumzo ambayo hakuyasikia na kuona vitu ambavyo hukuviona….” aliandika tena Tanasha.


Baadhi ya watumiaji wa mitandao walidai kwamba Tanasha alimuondoa (un-follow) Mondi, Mama Dangote na Esma miongoni mwa wafuasi wake kwenye Instagram.

Lakini cha kushangaza ni kwamba, malalamiko yaliyochapishwa na Tanasha yalijiri chini ya wiki mbili baada ya wawili hao kuachia wimbo wa pamoja wa Gere ambao hadi sasa umetazamwa zaidi ya mara milioni 9 kwenye Mtandao wa YouTube.

Katika wimbo huo, wawili hao wanaonekana wakiwazomea wale wanaouonea wivu uhusiano wao huku Tanasha akimsihi Mondi kutomsaliti.

HIZI HABARI ZA HIVI ZINAPATIKANA GODSTAR ONLINE >>BONYEZA HAPA KUDOWNLOAD APP YA GODSTAR ONLINE

No comments:

Post a Comment