Breaking

Monday, April 6, 2020

Bibi wa Miaka 100 Asotea Mafao Miaka 37

DAR: MIAKA 37 unasotea mafao serikali si jambo dogo, lakini bibi kizee, Edina Kambona ‘100’ mkazi wa Mbagala Kwamagai, Dar es Salaam, amekuwa katika hali hiyo kwa muda mrefu, Risasi Jumamosi lilifanya naye mahojiano.


Bibi Edina alisema mwishoni mwa wiki iliyopita kwamba, mafao hayo si yake bali ni ya mumewe aliyefariki akiwa kazini alipokuwa akifanya kazi Shirika la Ujenzi, mwaka 1983. 

Akielezea zaidi mkasa huo alisema, mumewe aliyekuwa akiitwa Sidwel Thawe alifanya kazi shirika hilo kwa miaka zaidi ya kumi na tano kabla ya kufariki dunia.


Alisema, mumewe akiwa kazini kwenye ujenzi wa barabara ya kutoka Songea Mjini kuelekea Tunduru eneo la Namtumbo mkoani Ruvuma hivi sasa, mumewe alipata ajali na gari la kazini na kupoteza maisha hapohapo.

“Kuanzia hapo nilianza kupata shida kwa kuwa nilikuwa nikimtegemea mume wangu karibu kwa kila kitu.

“Maisha yalianza kuwa magumu huku nikiwalea wanangu wawili alioniachia mume wangu.

“Baada ya muda nilianza kufuatilia mafao ambapo nilizungushwa ofisi mbalimbali serikalini bila mafanikio.
“Baadaye kuna mtu aliniambia niende Hazina nikafuatilie huko, nilielekezwa kwenda kwa mtu mmoja anaitwa Makame.
“Kweli nilikuta jina la mume wangu, jina langu na majina ya watoto wangu wawili, nikaona sasa ukombozi umepatikana.


“Baadaye Makame alianza kunisaidia kufuatilia mafao hayo, lakini cha ajabu mwishowe akaniambia, eti mafao ya mume wangu yalishatoka.

 

“Hapo tulianza kubishana nikitaka kujua kama yalitoka, basi nitajiwe aliyeyachukua, sikupewa jibu la uhakika.

“Tulirumbana sana lakini mwisho wa yote mpaka leo, bado sijapata hayo mafao nami naishi maisha ya dhiki,” alisema bibi Edina.

 
Aliongeza kuwa, tangu apatiwe majibu hayo, yapata takriban miaka 20 kuhangaika huku na kule kumtafuta mtu aliyechukua mafao hayo, lakini hadi leo hajafanikiwa.


Bibi huyo aliongeza kuwa, kutokana na mawazo na hali ngumu ya kimaisha, afya yake ilidhoofika na kujikuta akipatwa na tatizo la kupooza mwili na hivyo kufifisha kabisa ndoto za kupata haki ya marehemu mumewe.
“Sina fedha na wala sina mtu mwenye nguvu ya kusimamia jambo hili, hivi nimekutana na wewe mwandishi basi nimefurahi.

 
“Ombi langu ni kwa Rais Magufuli (John) anisaidie kupata haki, maana yeye ni mtetezi wa wanyonge na mimi ni mnyonge tena mnyonge hasa,” alisema bibi huyo kwa masikitiko.


Wakati huohuo mtoto wa bibi Edina ambaye ndiye anayemlea mama yake aliyejitambulisha kwa jina la Elizabeth Sidwel (61) alisema, amejaribu kuhangaikia mafao ya marehemu baba yake tangu akiwa msichana mpaka sasa na yeye amezeeka na kumekuwa hakuna matumaini yoyote.

Aliongeza kuwa, kinachowasikitisha zaidi ni uwepo wa taarifa kwamba mafao hayo yalishachukuliwa na mtu ambaye hafahamiki.


“Bora kungekuwa na tatizo la kisheria la sisi kupewa mafao ya baba yetu, lakini mtu asiyehusika kayachukua.

“Watu wana roho mbaya sana, wanamdhulumu mama yangu hadi jasho la marehemu mume wake,” alisema mtoto huyo.

Naye kwa upande wake, alimuomba rais Magufuli na viongozi wengine wa serikali hii ya awamu ya tano wawasaidie kupata haki yao ili angalau wapoze makali ya maisha hata katika kipindi hiki cha uzee wao.

HIZI HABARI ZA HIVI ZINAPATIKANA GODSTAR ONLINE >>BONYEZA HAPA KUDOWNLOAD APP YA GODSTAR ONLINE

No comments:

Post a Comment