Breaking

Saturday, April 18, 2020

Mwimbaji Zuchu Aonywa Kuhusu Diamond Platnumz

WATU bwana! Siku chache baada ya msanii chipukizi Zuchu Kopa kuachia albam yake fupi ‘EP’ iitwayo ‘I’m Zuchu’, wamemgeuzia kibao na kumuonya kwamba asipokuwa makini, bosi wake Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ au Mondi atampitia.

Zuchu ni memba mpya wa lebo ya Wasafi Classic Baby ‘WBC’ ambayo bosi wake ni Mondi anayeonywa kuishi naye kikazi zaidi ya mambo mengine.

“Huyu binti yuko safi sana kimuziki, mashaka yangu ni kwamba, Mondi anaweza kumfanya mrithi wa Tanasha Donna (mzazi mwenziye na Mondi),” mtu mmoja alikomenti kwenye mtandao wa kijamii wa Instagram.

Pekuapekua ya Risasi Mchanganyiko kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii imebaini ‘gari’ la Zuchu kisanii limewaka na kwamba amekuwa gumzo kila kona.

Hata onyo ambalo amepewa Zuchu, limetokana na wengi kukubali kazi zake na hivyo kumtahadharisha kuwa makini na safari yake ya kimuziki.

Pengine yote hayo yametokana na historia ya msanii Mondi kuwa ‘kiwembe’ kwa baadhi ya wasanii wa kike anaofanya nao kazi.

Inadaiwa kuwa, Mondi alianza uhusiano wa kimapenzi na Hamisa Mobeto, Irene Louis maarufu kama Official Lynn na Tunda Sebastian ‘Tunda’ baada ya kushirikiana nao kimuziki.

Hata hivyo, hiyo imekuwa kama mwangwi kwenye kazi nzuri ya I’m Zuchu aliyoiachia hivi karibuni ambayo imesheheni nyimbo kama Wana, Ashua na Hakuna Kulala. Nyingine ni Raha, Nisamehe, Kwaru na Mauzauza aliyoshirikiana na mama yake mzazi Khadija Kopa.

Miongoni mwa nyimbo hizo, Wana inafanya vizuri kwenye mtandao wa YouTube ambapo hadi gazeti hili linakwenda mtamboni, ulikuwa unasimama kwenye nafasi ya pili nyuma ya wimbo wa Dodo wa Ally Saleh Kiba ‘AliKiba’.

Kitakwimu Dodo wa Kiba ulikuwa umetazamwa na watu takriban milioni mbili huku ule wa Zuchu ukikimbiza na watu milioni 1.5 na hivyo kuweka hali ya hatari ya chipukizi huyo kuweza kumshusha mkongwe Kiba kwenye chati.

Zuchu alianza kazi ya sanaa mwaka 2018 akisimamiwa na WCB huku kipaji chake kikionekana kuchanua toka aliposhiriki Shindano la Tecno Own Stage ambalo hata hivyo hakushinda.

Mwaka 2020 bosi wa WCB, Mondi alimtambulisha rasmi Zuchu kuwa memba kamili wa lebo hiyo na fasta kuachia EP yake ambayo imeanza kuunguza vichaka vya mastaa wakongwe kwenye gemu ya muziki wa Bongo Fleva.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kupitia ukurasa wake wa Instagram, aliweka ujumbe wa pongezi kwa Zuchu.

Aidha, pongezi zaidi alizimwaga kwa Diamond na kumweleza bosi huyo wa WCB kuwa ni muda umefika kwa mkurugenzi huyo wa lebo ya Wasafi kuanzisha chuo cha muziki nchini.

Gazeti hili lilimtafuta Zuchu ili azungumzie ishu ya onyo analopewa na wadau wake, hakuweza kupatikana lakini meneja wake Hamisi Shaban Taletale ‘Babu Tale’ alipotafutwa aliishia kummwagia sifa msanii huyo.

“Tumetumia takriban miaka minne kumpitisha huyu Zuchu, tunaamini anakuja kuleta mapinduzi kwenye muziki,” alisema.

Wakati huohuo mama mzazi wa Mondi, Sanura Kassim ‘Sandra’ kupitia ukurasa wake wa Instagram alimmwagia sifa Zuchu huku akienda mbali zaidi kwamba hata akipasuliwa mwili, Zuchu atakutwa ndani ya damu yake.

STORI | Memorise Richard, Risasi

HIZI HABARI ZA HIVI ZINAPATIKANA GODSTAR ONLINE >>BONYEZA HAPA KUDOWNLOAD APP YA GODSTAR ONLINE

No comments:

Post a Comment