Breaking

Sunday, April 26, 2020

Tetesi za Mwanamuziki Ray Vanny Kujitoa Lebo ya WCB Wasafi....


DAR: Kruu ya Wasafi Classic Baby (WCB), limeendelea kuwa chanzo kikubwa cha habari za mastaa Bongo, safari hii kuna mpya inayomhusu bwa’mdogo mwenye Mbeya yake mgongoni, Raymond Mwakyusa ‘Rayvanny’ au unaweza kufupisha kwa kumuita Vanny Boy kama siyo Vanny peke yake, IJUMAA linakushushia habari kamili.

HABARI YENYEWE

Habari ikufikie kuwa, kuna viashiria vya kutosha vinavyoonesha kwamba staa huyo anayesumbua na Wimbo wa Miss Buza alioshirikiana na Dulla Makabilia, huwenda akajitoa, ana tatizo au tayari hayupo WCB.

“Nahisi kuna tatizo, ninyi kwa vile najua mnajua namna ya kuchimba habari zenu, chimbeni tu mtaupata ukweli,” chanzo makini kililipenyezea ubuyu Gazeti la IJUMAA.

Kama hiyo haitoshi, chanzo hicho kilikwenda mbele zaidi kwa kusema huwenda msanii huyo akatimkia kwenye Lebo ya Konde Gang inayomilikiwa na aliyekuwa memba wa WCB, Rajab Abdul ‘Harmonize’.

“Nasikia anaweza kwenda huko kwa Harmonize ninyi fuatilieni tu mtabaini ukweli,” kilisema chanzo hicho.

 
UCHUNGUZI FASTA

Bila kupoteza muda, Gazeti la IJUMAA, baada ya kumegewa ‘info’ na chanzo hicho cha kuaminika, fasta lilianza uchunguzi wake ambao ulibaini kuna jambo kati ya msanii huyo na WCB.

JAMBO LA KWANZA

Awali ya yote, IJUMAA lilijiridhisha pasi na shaka, kwa siku za hivi karibuni bosi wa WCB, Nasibu Abdul ‘Mondi’ amekuwa hasapoti kazi za Vanny kama anavyofanya kwa msanii wake mwingine wa Wasafi, Mbwana Yusuf Kilungi ‘Mbosso’.

Zamani ilikuwa, Vanny akitoa ngoma au kufanya jambo lolote, lazima Diamond atashadadia iwe ni kwa utani au ‘serious’.

MAHABA KWA MBOSSO

Lakini IJUMAA pia lilishuhudia ndani ya kipindi hicho ambacho hamsapoti Vanny, sasa amehamisha mahaba kwa Mbosso.

Amekuwa akisapoti kazi zake kwa ukaribu zaidi sanjari na msanii wake mpya aliyemsajili hivi karibuni, Zuhura Kopa ‘Zuchu’.

MTU WA NDANI ANENA

Gazeti la IJUMAA lilizungumza pia na mtu aliye ndani ya Kruu ya Wasafi ambaye alikiri kuwepo na sintofahamu juu ya Rayvanny.

“Kwa kweli kutakuwa na kitu maana kweli simuoni mkubwa akimsapoti Vanny kwa sasa,” alisema mtu huyo aliyeomba hifadhi ya jina.

RAYVANNY ANASEMAJE?

Ili kuanza kupata ukweli wa mambo, IJUMAA liliamua kumvutia waya Rayvanny ili kumsikia anazungumziaje taarifa hizo.

MAJIBU YA KUSHANGAZA

Tofauti na matarajio, licha ya IJUMAA kupiga namba ambayo imesajiliwa kwa jina la Raymond Mwakyusa, mtu aliyepokea alitoa majibu ya kushangaza kwa kujibu kirahisi sana.

“Eee ndiyo ni kweli, nimeondoka Wasafi, nakwenda Konde Gang,” alisema mtu huyo aliyepokea simu ya Rayvanny.

IJUMAA lilishindwa kupata majibu ya moja kwa moja, je, msanii huyo ameacha kuitumia namba hiyo? Au amempa mtu apokee? Au vinginevyo? Jibu atakuwa nalo mwenyewe.

MAMENEJA WASAKWA

Baada ya kukusanya taarifa hizo, IJUMAA liliingia mzigoni na kuwatafuta mameneja wa lebo hiyo ili kuweza kupata ukweli juu ya jambo hilo.

Wa kwanza alikuwa ni Said Fela maarufu kwa jina la Mkubwa na Wanawe ambaye alisema hawezi kumzungumzia Rayvanny kwani hajamuona msanii huyo kwa muda.

“Mimi sina taarifa zozote kuhusiana na Rayvanny kujitoa Wasafi na wala sijaonana naye kwa hiyo siwezi nikasema habari ambazo sina taarifa nazo.”

BABU TALE JE?

Baada ya kumalizana na Fela, IJUMAA lilimvutia waya Hamis Taletale ‘Babu Tale’ ambaye pia ni Meneja wa Wasafi ili aweze kuthibitisha taarifa hizo ambapo yeye alisema kuwa habari hizo ni ngeni kwake.

“Mimi ndiyo nazisikia taarifa hizi sizijui kabisa sasa hivi watu wapo bize na Corona maana ugonjwa umekuja kila mtu afuate taratibu ambazo zimewekwa na mamlaka husika ili uishe tuendelee na kazi maana hali ni mbaya kila kona,” alisema Babu Tale.

NI BAADA YA HARMONIZE

Tetesi za Vanny kutaka kujitoa Wasafi zilianza kuvuma punde tu baada ya Harmonize kujitoa na kwenda kuanzisha lebo yake.

Mbali na Harmonize, kundi hilo pia liliwahi kuondokewa na msanii wao mwingine, Richard Martin ‘Rich Mavoko’ ambaye kwa sasa amepoa kimuziki.

Stori: NEEMA ADRIAN, Ijumaa

HIZI HABARI ZA HIVI ZINAPATIKANA GODSTAR ONLINE >>BONYEZA HAPA KUDOWNLOAD APP YA GODSTAR ONLINE

No comments:

Post a Comment