Breaking

Thursday, April 23, 2020

Wasafiri wanaopita Morogoro Wote Kupimwa Afya zao

SERIKALI mkoani Morogoro, imeazimia kusimamisha magari yote yanayopita ndani ya mkoa huo yakiwemo ya abiria ilikuwapima abiria ikiwa ni moja ya njia ya kukabili maambukizi ya virusi vya corona kuendelea kusambaa nchini.

Agizo hilo lilitolewa jana na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Loata Sanare, kwenye kikao cha wadau wa mkoa huo kwa kilichokuwa na lengo la kuweka mikakati ya namna ya kukabiliana corona.

Sanare alisema hatua hiyo hailengi kuwazuia wasafiri kuingia au kupita Morogoro bali inalenga kujua afya zao na kuwakinga wengine hususani wananchi wa Mkoa wa Morogoro.

“Tumetembelea maeneo mbalimbali jana ikiwepo Mikese, tuna kituo kule tunaweza tukatumia kuwapima madereva wote wanaokuja, tunavyo vifaa vya kuwapima joto, sio kuwazuia lakini tujue usalama wao” alisema Loata Sanare.

Kutokana na hali hiyo, alimtaka Mganga Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dk. Kusilye Ukio, kuandaa utaratibu wa kupima dalili za ugonjwa huo kwa wasafiri wote wanaoingia Manispaa ya Morogoro.

Sanare pia alitoa wito kwa wadau hao kutoa michango ya kukabiliana na homa hiyo wito ambao ulipokelewa na wengi wao waliahidi kutoa fedha, vifaa tiba na vifaa kinga.

Aidha alisema kwa kuwa jambo hilo linatakiwa kufanyika kwa haraka, wadau wawe na siku maalum kwa kutoa michango kama walivyoahidi na kwamba Aprili 24 mwaka ndiyo siku ya wote kutoa michango waliyoahidi.

Pia alitoa onyo kwa wadau hao akiwataka wote kutekeleza maagizo ya Serikali na ushauri unaotolewa na wataalamu wa afya katika jitihada za kutokomeza gonjwa huo.

Wajumbe wa kikao hicho, kwa nyakati mbalimbali wakichangia mjadala huo walishauri Serikali iongeze jitihada za kuzuia mikusanyiko ya watu isiyo ya lazima katika maeneo mengi ndani ya Mkoa huo hususani katika Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro kwa kuwa wengi wanaonekana kutotilia maanani suala zima la kuwa na tahadhari yahoma hiyo.

Naye Mmiliki wa vyombo vya habari vya TV Imani, Redio Imani na gazeti la Imani (Islamic foundation) Aref Nahd alishauri vyombo vya habari vitumike katika kuendelea kusisitiza masuala yanayotolewa na Serikali ya kujikinga na corona watu wengi watapata elimu ya kujikinga na ugonjwa huo.

Askofu wa Jimbo Katoliki la Morogoro, Telesphori Mkude alimshukuru mkuu wa mkoa kwa kuandaa kikao hicho kilichowapa ufahamu wa hali ya ugonjwa wa corona mkoani humo na kupata elimu ya namna ya kujikinga.

HIZI HABARI ZA HIVI ZINAPATIKANA GODSTAR ONLINE >>BONYEZA HAPA KUDOWNLOAD APP YA GODSTAR ONLINE

No comments:

Post a Comment