Breaking

Sunday, May 17, 2020

Msoto wa Amber Lulu Kwenye Maisha ni Fundisho Tosha

UKIMUONA leo kila anapokatiza mitaani, hakika jina lake lipo vichwani mwa mashabiki wake.Si kwamba tu watu watamtazama kutokana na ile shepu yake ambayo hata yeye anajivunia, lakini ni namna alivyoweza kutoboa kwenye sanaa na kufanikiwa kuzikonga nyoyo zao.

 

Ameonekana na kusikika kwenye nyimbo mbalimbali kama Jini Kisirani, Leo Watakoma na nyingine kibao akitokea kwenye mkumbo wa video vixen walioingia kwenye muziki.
Huyu hapa Lulu Euggen ‘Amber Lulu’.

 

Pamoja na vitu vingi alivyonavyo, lakini nyuma yake kuna msoto mkali alioupitia kiasi ambacho kwa mwingine angekata tamaa kirahisi.

 

Gazeti la IJUMAA kama kawaida yake limepiga stori nyingi na Amber Lulu ambaye anaeleza mambo aliyokutana nayo kabla ya kufanikiwa kutoboa.IJUMAA: Kulikoni mbona kimya sana?

AMBER LULU: Sasa hivi hakuna mwenye ujanja kutokana na janga hili la Corona, yaani ni shida tupu. Tumebaki tu kumuomba Mungu mtu ulale kisha uamke ukute janga hili limepita ili mambo mengine yaendelee.

IJUMAA: Kwa upande wako Corona imekuathiri kwa kiasi gani?

 

AMBER LULU: Madhara siyo ya kuuliza, kwani yanaonekana kila kona kwenye maisha yetu, kila kitu kimekaa hovyo. Kwa mtu kama mimi ilikuwa ni lazima nifanye shoo ndipo mambo yaende kwa sababu sina kitu kingine cha kuniingizia kipato, maisha yangu yote ni muziki na mimi.

 

IJUMAA: Baadhi ya watu wanaweza kusema labda umeibuka tu kwenye muziki na hukupitia msoto wowote. Je, ni kweli?

AMBER LULU: Niseme ukweli, nimesikia stori za mastaa wengi ndani na nje ya Bongo, lakini mimi nimepita kwenye msoto mkubwa sana usione hivi. Kuna mwingine anaona ni rahisi sana, lakini mambo hayakuwa hivi yalivyo.

IJUMAA: Ni msoto gani, uweke wazi ili watu wajifunze kupitia kwako.

 

AMBER LULU: Nilianza kujitafutia maisha nikiwa msichana mdogo sana kwa sababu mama yangu alipata tatizo, hivyo hakuweza kumudu mahitaji yetu. Nakumbuka kipindi hicho niko Mbeya na familia yangu, maisha yalikuwa magumu sana. Nilianza kutumia kichwa changu kuona wapi nitapata msaada. Kiukweli naomba niseme tu kwa kifupi kwamba, haikuwa kazi rahisi kufika hapa, nikisema nisimulie hatua kwa hatua tutalijaza Gazeti la IJUMAA na kunikumbusha machungu mengi.

 

IJUMAA: Ili kufikia ndoto zako za kuwa mwanamuziki, ulihitaji msaada gani?

 

AMBER LULU: Kabla ya yote na kuja kuwa hivi nilivyo, nilihitaji sana msaada ili kujikimu mimi na mama yangu maana alikuwa anaumwa. Kwa kuwa nilikuwa ninapenda muziki na ndiyo ilikuwa ndoto yangu, nilianza kutafuta namna ya kutoka.IJUMAA: Bado hatujapata picha ya jinsi ulivyohaso hadi ukafika Dar kutoka Mbeya…

 

AMBER LULU: Hapa Dar nilifika kwa kuungaunga. Nilikuwa nimeshaamua kwamba lazima nitoboe kwenye muziki kwa namna yoyote ile. Nilipofika hapa Dar, maisha yangu yalikuwa ya kwenye mageto tu. Huko nilikutana na kila aina ya watu. Huko ndiko nilikokomaa akili nilijulikana, lakini siyo mazuri.

 

Ilifika kipindi nikipita mitaani ninajifunika uso kwa sababu kwa bahati mbaya hata usafiri nilikuwa sina.IJUMAA: Ulipokuwa ukifanya hivyo, ulikuwa unapenda?

 

AMBER LULU: Kiukweli kabisa nilikuwa sipendi, lakini nilijivika tu moyo mgumu ili tu nitoboe na kutoboa kwangu watu walikuwa hawanielewi. Hata zilipovuja picha zangu nyingine nikiwa mtupu kabisa ambazo mwanaume alirekodi mapema mno. Nilijikuta kwenye mkumbo wa ili nitoboe, lazima niachie picha chafu.
 

IJUMAA: Nani alikupa wazo hilo na hukuona kama ni kinyume cha maadili?

AMBER LULU: Niliona kila ninalofanya sifanikiwi. Nilishajiita majina yote, lakini bado sikutoboa. Nilianza kuachia picha zangu kutokana na ushawishi wa mabinti wenzangu niliokuwa nikiishi nao mageto. Kiukweli picha zile zilisaidia kidogo, ghafla nilianza kujulikana. Najua na kuziposti kwenye mitandao, hapo ndipo akili yangu ikakaa sawa na kurudi nyuma kasi na kuona ninaweza kutoboa hata bila kujidhalilisha kiasi kile.

 

IJUMAA: Kipindi chote hicho ndugu zako hasa mama yako mzazi alikuchukuliaje?

 

AMBER LULU: Nilisahau kidogo, wakati nikiendelea kutafuta namna ya kutoka, kwa bahati mbaya mama yangu alifariki dunia kabla ya kuona mafanikio yangu. Iliniuma sana! Hapo hata ndugu zangu sikutaka kuwapa nafasi, niliona watanichanganya tu, nikaziba masikio.IJUMAA: Kutokana na msoto huo, kuna ulilojifunza hadi hapa ulipo?

 

AMBER LULU: Nimejifunza mengi sana, lakini kubwa niwaambie mabinti au wanawake wenzangu kuwa, siyo lazima upige picha chafu ndiyo ujulikane. Nimejifunza picha chafu zinadhalilisha sana tu na hupati heshima inayotakiwa kabisa.

 

IJUMAA: Kwa sasa umetulia sana na makeke yako hayaonekani mitandaoni kama zamani, nini kimetokea?
 

AMBER LULU: Nipo, lakini kukiwa na jambo ambalo ni muhimu kwa mashabiki wangu.IJUMAA: Kipindi cha nyuma kulikuwa na madai ya wewe kutoka kimapenzi na Young D na ulikuwa unaishi naye, vipi uhusiano wenu bado upo?
AMBER LULU: Kwa kweli kila mtu ana maisha yake sasa. Unajua kuna vitu vingine ni vya ujana zaidi.

 

IJUMAA: Vipi kuhusiana na madai ya kutumia madawa ya kulevya na ulevi wa kupitiliza?

AMBER LULU: Hakuna lenye mwanzo lisilo na mwisho. Kuhusu madawa ya kulevya si kweli, ila pombe ni kweli nilikuwa nakunywa sana, lakini sasa basi.

Makala: Imelda Mtema, Bongo

HIZI HABARI ZA HIVI ZINAPATIKANA GODSTAR ONLINE >>BONYEZA HAPA KUDOWNLOAD APP YA GODSTAR ONLINE

No comments:

Post a Comment