Breaking

Friday, June 5, 2020

Wolper Amfunika Wema kwa Wachumba

 

WIKIENDI iliyopita staa wa sinema za Kibongo, Jacqueline Wolper Massawe mwenye umri wa miaka 33, amechumbiwa na mfanyabiashara wa nguo jijini Dar, Rashid almaarufu kama Chid Designs na kuvunja na kuweka rekodi kwenye ulimwengu wa mastaa wa Bongo, RISASI MCHANGANYIKO lina ripoti kamili.

Miongoni mwa yanayozungumzwa zaidi na mashabiki wake baada ya tukio hilo lililofanyika dukani kwa Wolper, Sinza-Makaburini jijini Dar ni kwamba, sasa amemfunika staa mwenzake wa sinema za Kibongo, Wema Isaac Sepetu kwenye kipengele cha kuwa na idadi kubwa ya wachumba.

Awali, ilifahamika kwamba, wote wawili, Wolper na Wema walikuwa na idadi sawa ya wanaume waliowachumbia ambapo kila mmoja alikuwa nao watatu, lakini sasa Wolper yeye ana wanne baada ya kuchumbiwa na Chid.

Watu mbalimbali wameendelea kumpongeza Wolper kwa tukio hilo, kwani amepitia changamoto nyingi za kuchumbiwa na kuachwa solemba.

“Namshukuru Mungu kwa kila kitu na yeye ndiye muweza wa yote…

“Mungu aliyepanga, ndiye anajua kila kitu kuhusu hili na atasimamia haya na kila kitu kitakwenda kwa mipango yake, nachoma mambo yangu yote ya zamani na kuanza mwanzo mpya na Mungu akanitengeneze kuwa mke kama alivyopanga yeye na akatutengeneze mimi na mchumba wangu tukawe anavyopenda yeye na siyo mimi wala watu.

“Nawashukuru wote mlionipongeza na kuwa karibu na mimi, Mungu awabariki sana.

“Siwezi kujibu kila mmoja, lakini naona comments (maoni) zenu. Asanteni dada zangu na marafiki zangu kwa ujumla,” aliandika Wolper kwenye ukurasa wake wa Instagram.

WACHUMBA WA WOLPER

Huko nyuma, gazeti hili linafahamu kuwa, aliwahi kuchumbiwa na mfanyabiashara maarufu jijini Dar, Abdallah Mtoro ‘Dallas’, lakini mambo hayakwenda sawa, kwani waliachana ndani ya muda mfupi.

Taarifa zilizopo kwenye makabrasha ya gazeti hili yanaonesha kuwa, baada ya hapo, Wolper alichumbiwa na mfanyabiashara, raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo aliyeitwa Putin almaarufu Mkongo wa Wolper ambaye alimhamisha Bongo na kwenda kuishi naye nchini Afrika Kusini, lakini miezi kadhaa mbele, mrembo huyo alirejea Bongo na maumivu kama yote.

Baada ya hapo, mwaka 2018, Wolper alichumbiwa na mwanaume wa tatu aitwaye Sadick Athanas Sanga ‘Engine’ ambaye alikwenda naye hadi kijijini kwao, Moshi na msafara mkubwa wa magari kutoka Dar.

Hata hivyo, juu ya nini kilitokea kati ya Wolper na Sanga imebaki kuwa stori ya maumivu kwenye moyo wa malkia huyo wa mavazi na sasa yupo mikononi mwa Chidi ambaye ni mchumba’ke wa nne.

WACHUMBA WA WEMA

Kwa upande wake Wema, inafahamika kuwa, wakati akiwa kwenye mapenzi shatashata na aliyekuwa staa wa filamu za Kibongo, marehemu Steven Kanumba, ghafla zilianza kusikika tetesi kuwa anataka kuchumbiwa na mwanaume aliyeitwa Jumbe Yusuf Jumbe.

Hata hivyo, wakati mambo yakiwa ni moto, wawili hao walitangaza kuvishana pete za uchumba na mipango ya ndoa kuanza kabla ya mama wa mrembo huyo, Mariam Sepetu kuingilia kati na kumchukua mwanaye mikononi mwa jamaa huyo kwa kutumia nguvu ya ziada ambapo ilibidi Wema atupwe rumande ili kuweka akili yake sawa.

Kutoka kwa Jumbe, pia Wema alisemekana kuchumbiwa na aliyekuwa mwimbaji wa Bendi ya Machozi aliyejulikana kwa jina la Mwinyi.

Wakati Wema anachumbiwa na Mwinyi, alikuwa ametoka kuachana na staa wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’.

Hata hivyo, wakati watu wakisubiria ndoa, ghafla zilisikika tena kelele za Wema kurejea kwa Diamond na huo ukawa ndiyo mwisho wa uchumba wake na Mwinyi.

Mara baada ya kurejea kwa Diamond, fastafasta jamaa huyo alimvisha Wema pete ya uchumba ambao ulikutana na misukosuko kutoka kila upande kiasi cha kufikia ukingoni.

Kwa sasa Wema hajatangaza kuwa na mchumba mwingine.

WOLPER AWEKA REKODI

Kwa mujibu wa wachambuzi wa duru za mastaa ndani na nje ya Bongo, Wolper ameweka rekodi ya kuwa na wachumba wengi kuliko staa mwingine yeyote Bongo.

Wadau wake wameliambia Risasi Mchanganyiko kuwa, Wolper ndiye staa pekee Bongo kipenzi chao ambaye ameweza ‘kumeinteini’ jina lake bila kushuka ndani ya Bongo, lakini suala la kuwa na mwanaume wa kueleweka, limekuwa likimuumiza kichwa.

WOLPER ANASEMAJE?

Gazeti hili lilimtafuta Wolper ili kujua anazungumziaje maisha yake mapya na Chid ambapo alikuwa na haya ya kusema;

“Namshukuru Mungu kwa sababu mara nyingi ninakosewa mimi, lakini naonekana mshenzi.

“Nilisema this time (safari hii) nita-date (nitakuwa kwenye uhusiano wa kimapenzi), lakini sitaposti mitandaoni wala sitatoa ruhusa nipostiwe ili yasitokee yalele.”

MBALI NA WACHUMBA

Mbali na kuwa na rekodi ya idadi hiyo ya wachumba, pia Wolper aliwahi kutajwa kwenye uhusiano na mastaa mbalimbali kama Jux, Kiba, Diamond, Harmonize, Young Killer, Brown na wengineo.

STORI | Mwandishi Wetu, Risasi

HIZI HABARI ZA HIVI ZINAPATIKANA GODSTAR ONLINE >>BONYEZA HAPA KUDOWNLOAD APP YA GODSTAR ONLINE

No comments:

Post a Comment